1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri wa Nje wa Ujerumani ziarani Mashariki ya Kati

24 Novemba 2009

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Guido Westerwelle wakati wa ziara yake ya saa mbili Ukingo wa Magharibi leo hii amewataka Waisrael na Wapalestina kurudi katika meza ya mazungumzo ya amani kwa haraka iwezekanavyo.

https://p.dw.com/p/KeAG
In this image made available by the Israeli Government Press Office, Israeli Prime Minister Benjamin Netanyahu, left, sits next to German Foreign Minister Guido Westerwelle during their meeting in Jerusalem, Monday, Nov. 23, 2009. Westerwelle is on an official visit to the region. (AP Photo/Moshe Milner, GPO) ** ISRAEL OUT ** ISRAEL OUT AP PROVIDES ACCESS TO THIS PUBLICLY DISTRIBUTED HANDOUT PHOTO TO BE USED ONLY TO ILLUSTRATE NEWS REPORTING OR COMMENTARY ON THE FACTS OR EVENTS DEPICTED IN THIS IMAGE
Guido Westerwelle kushoto akutana na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: AP
Katika ziara yake hiyo ya Mashariki ya Kati Westerwelle amesema Ujerumani ina wajibu maalum kwa Israel. Kaimu Waziri Mkuu wa Wapalestina Salama Fayyad amesema baada ya kukutana na Westerwelle mjini Ramallah kwamba waziri huyo wa mambo ya nje wa Ujerumani anaunga mkono madai ya Wapalestina ya kusitishwa kabisa kwa ujenzi wa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi katika maeneo yote yanayokaliwa kwa mabavu na Israel ikiwa ni pamoja na Jerusalem ya Mashariki. Fayyad ameuambia mkutano wa waandishi wa habari kwamba wamezungumzia matakwa ya mpango wa ramani ya amani ambapo Israel inapaswa kusitisha harakati zote za ujenzi wa makaazi katika maeneo yote na kwamba kulikuwa na makubaliano na waziri huyo wa Ujerumani juu ya jambo hilo. Serikali ya Ujerumani ilielezea kusikitishwa kwake sana na uamuzi wa Israel kujenga makaazi katika ardhi ilioinyakua na kuikalia kwa mabavu katika vita vya mwaka 1967 na kuijumuisha kwenye mipaka ya manispaa ya Jerusalem. Ujerumani inaona ujenzi wa makaazi hayo kuwa kikwazo kikubwa katika njia ya kusonga mbele na mchakato wa amani. Westerwelle amesema lazima wachukuwe hatua zote kufufua mchakato huo wa amani haraka. ´´Tunachotaka ni ufumbuzi wa kuwepo kwa mataifa mawili kwanza Israel ina haki ya kuishi katika mipaka salama na wakati huo huo Wapalestina wawe na haki ya kuishi katika taifa lao´´. Waziri huyo mpya wa mambo ya nje wa Ujerumani alifanya safari hiyo fupi huko Ramallah akitokea Jerusalem ambapo baada ya kuwasili kwake hapo jana alitembelea kumbukumbu ya Maangamizi ya Wayahudi ya Yad Vashem kabla ya kuwa na mazungumzo na waziri wa mambo ya nje wa Israel Avigdor Lieberman hapo jioni. Akitembelea eneo la kumbukumbu ya Maangamizi ya Wayahudi ya Yad Vashem ya Wayahudi milioni sita waliouwawa na Manazi wa Ujerumani wakati wa Vita Vikuu vya Pili Westerwelle amesema Ujerumani ina wajibu maalum kwa Israel. Ziara ya Westerwelle Mashariki ya Kati inakuja wiki moja kabla ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kukutana mjini Berlin na Kansela Angela Merkel na mawaziri wa Israel na Ujerumani kuwa na kikao cha pamoja. Ziara yake inafanyika wakati kukiwa na repoti za juhudi mpya na hata uwezekano wa kufikiwa makubaliano katika mazungumzo yanayosuluhishwa na Ujerumani ya kumuachilia huru askari wa Israel anayeshikiliwa na kundi la Hamas la Wapalestina kwa zaidi ya miaka mitatu katika Ukanda wa Gaza. Waziri wa mambo ya nje wa Israel Lieberman akikutana na Westerwelle hapo alimshukuru waziri mwenzake kwa juhudi za serikali ya Ujerumani kufanikisha makubaliano hayo akisema kwamba bado haiko wazi iwapo kutafikiwa kwa makubaliano ya kubadilishana wafungwa kati ya Israel na kundi hilo la Hamas. Westerwelle mwenyewe hakutoa ufafanuzi juu ya juhudi hizo za Ujerumani akisema tu anatumai yatapelekea kupatikana kwa matokeo mazuri kwa kuzingatia mtizamo wa kibinaadamu. Ziara hiyo ya Westerwelle nchini Israel ni ya kwanza tokea ashike wadhifa wake huo mpya mara ya mwisho aliitembelea Israel miaka saba iliopita wakati akiwa mwanasiasa wa upinzani. Ziara yake hiyo ilitiwa kiwingu na matamshi ya mwenzake kutoka chama cha Free Democratic Juergen Moellermann ambayo yalionekana kama dhidi ya Uyahudi na kushindwa kwa Westerwelle kujitenganisha haraka na matamshi hayo. Mwandishi:Mohamed Dahman/DPA Mhariri:M.Abdul-Rahman