1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri wa ulinzi wa Marekani Gates awasili Irak

1 Septemba 2010

Askari 50,000 wa Marekani watakuwa chini ya wizara ya nje

https://p.dw.com/p/P1Zc
Waziri wa ulinzi Robert GatesPicha: AP

Kufuatia tangazo la Rais Obama kuwa Marekani imemaliza vita vyake nchini Irak, waziri wake wa ulinzi, Robert Gates, amewasili leo Baghdad, akifuata nyayo za makamo-rais Joe Biden, ambae tangu juzi Jumatatu yupo nchini Iraq akizungumza na wanasiasa wa nchi hiyo. Idadi ya watu waliouwawa nchini Iraq mwezi wa August uliomalizika jana imepungua kidogo kutoka ile ya mwezi uliotangulia.

Kwa muujibu wa maafisa wa Marekani mjini Baghdad, waziri wa ulinzi, Robert Gates, atakutana na waziri-mkuu, Nuri al-Maliki, maafisa wa ulinzi na viongozi wa juu wa kijeshi.Ziara yake imesadifu kutokea wakati mmoja na ile ya makamo-rais Joe Biden, aliewasili Baghdad tangu Ijumatatu.

Baadae, Jamadari Raymond Odierno wa Marekani, atamkabidhi usimamizi wa kikosi cha askari 50.000 wa Marekani, mfuasi wake Jamadari Lloyd Austin, ambae atakuwa na jukumu la kusimamia mafunzo na harakati za kupambana na ugaidi. Jukumu hilo jipya kwa kikosi hicho kwa jina la "New Dawn" litakuwa chini ya uongozi wa wizara ya nje ya Marekani.

Taarifa zilizochapishwa leo mjini Baghdad kuhusu idadi ya waliouwawa mwezi uliomalizika wa August inaonesha idadi yao imepungua kutoka ile ya mwezi uliotangulia-Julai. Jumla ya watu 295 waliuwawa mwezi uliopita kupitia miripuko ya mabomu na ufyatuaji risasi- hii ni kwa muujibu wa tarakimu za wizara ya siha ya Iraq. Idadi ya raia waliouwawa Julai ilikua 396. Idadi ya waliofariki ilikuwa kubwa hapo Julai, mwaka huu na hasa miongoni mwa vikosi vya Iraq. Wanajeshi 54 na polisi 77 waliouwawa katika hujuma za waasi.

Wakati Rais Barack Obama, amesema anafungua ukurasa mpya juu ya usuhuba kati ya Marekani na Irak, aliekuwa mshirika wa chanda na pete wa vita vya Marekani nchini Irak wakati wa enzi ya utawala wa George Bush, waziri-mkuu wa zamani wa Uingereza, Tony Blair, amechapisha leo kumbukumbu zake. Humo Blair, ameungama kwamba, hakuota jiinamizi lililokuja kuikumba Iraq, hata hivyo, hana majuto kwanini alijiunga na uvamizi uliongozwa na Marekani nchini Iraq.

"Sijutii uamuzi wa kwenda vitani......lakini naweza kusema sikutumai kungezuka balaa lililoikumba Irak ."

Blair katika kumbukumbu zake aliongeza,

"Mara nyingi nikiwaza iwapo nilifanya makosa. Nawaombeni muwaze nanyi iwapo huenda sijakosea."

Kuanzia jana ,waziri-mkuu wa Iraq, Nuri al-Maliki, amenadi kuwa Iraq, imerudisha uhuru na mamlaka yake tangu sasa hata kwa mustakbala wake unaokuja. Usuhuba na Marekani, alisema, utakuwa zaidi wa ushirikiano wa kiuchumi na diplomasia kuliko kijeshi.

Mwandishi: Ramadhan Ali/DPAE/RTRE

Uhariri: Miraji Othman