1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ziara ya Westerwelle nchini China

Abdu Said Mtullya15 Januari 2010

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Guido Westerwelle anaendelea na ziara ya barani Asia kwa kuitembelea China.

https://p.dw.com/p/LXHL
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Guido Westerwelle ziarani China.Picha: AP

Waziri  wa  mambo ya nje  wa Ujerumani, Guido    Westerwelle, alieanza  ziara nchini China leo , amefanya mazungumzo  na waziri mwenzake juu    ya masuala  ya haki  za binadamu  vilevile.

Waziri Westerwelle  amesema masuala  ya uhuru  wa vyombo  vya  habari na uhuru  wa kutoa maoni ni sehemu ya msingi wa  sera za nje  za Ujerumani.

Waziri Westerwelle anaefanya  ziara ya China  kwa mara  ya  kwanza  tokea ashike wadhifa  wa  waziri wa  mambo  ya nje ameashiria    uwezekano  wa  kukutana  na kiongozi  wa  kidini  anaepigania  uhuru wa Tibet, Dalai Lama . Waziri  Westerwelle ambae  leo  alikutana  na waziri mkuu  wa China  Wen Jiabao, amesema   kwamba tayari  ameshawahi  kuwa  na  fursa ya kukutana  na Dalai Lama mnamo  siku za nyuma.

Hata hivyo, ameeleza  kwamba  kwa  sasa hakuna mkutano uliopangwa kufanyika baina yake na kiongozi huyo wa kidini.

Waziri Westerwelle na waziri mwenzake, Yang Jiechi, walifanya  mazungumzo  na walipeana mawazo  juu  ya suala  la Tibet. Waziri Yang  alimwambia  mgeni wake kutoka  Ujerumani kwamba China  inapinga mawasiliano yote  baina  ya Dalai Lama na viongozi wa nchi za  nje. Mawaziri  hao pia walijadili suala  la Iran. China imesisitiza kwamba  yapo masuala  muhimu  sana, lakini China  inataka  kuletwa  suluhisho  kwa njia  ya  mazungumzo.

Kwa upande wake, waziri  Westerwelle amesema   mipango yoyote  ya Iran ya kuunda  silaha  za  nyuklia haitakubalika  na kwamba Ujerumani ipo tayari  kuiwekea nchi hiyo  vikwazo zaidi ikiwa mazungumzo yanayofanyika  sasa yatashindikana.

Mwandishi/Mtullya Abdu/ ZA AFP.

Mhariri: Miraji Othman