1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wazuwia uhalifu Uganda wamulikwa

Admin.WagnerD13 Januari 2016

Mashirika kadhaa ya haki za binaadamu yameitaka serikali ya Uganda kusitisha mara moja kile kinachojulikana kama Mpango wa kuzuwia uhalifu, wakati ikielekea kwenye uchaguzi mkuu tarehe mwezi ujao

https://p.dw.com/p/1HcLr
Kampala Uganda Straße Taxi Busse
Kampala, UgandaPicha: Getty Images/ I. Kasamani

Mashirika yaliotoa wito huo kuitaka serikali ya Uganda isitishe mpango huo ni Shirika la Kimataifa la Haki za Binaadamu -Amnesty International. Human Rights Watch, Mtandao wa Haki za Binaadamu Uganda-HURENITE-U, Chapter four Uganda na Foundation for Human Rights Initiative. Kimsingi kundi hilo linalioitwa "Wanaozuwia uhalifu," linamafungamano makubwa na Chama tawala cha National resistance-NRM na wanachama wa kundi hilo huendesha harakati zao wakijihusisha na NRM. Mashirika ya haki za binaadamu yanasema Visa vinavyoripotiwa ni pamoja na kuwapiga watu kikatili bila ya kuwajibishwa.

Mtafiti mmoja wa ngazi ya juu anayehusika na Afrika katika Shirika la Human Rights Watch Maria Burnett amesema, kimsingi kutumiwa makundi hayo ya kujitolea kufanya shughuli za ulinzi kwa niaba ya jamii sio jambo jipya , lakini yanapaswa kuwa yasioelemea upande wowote kisiasa, kupewa mafunzo sahihi na yawajibike ipasavyo na sio vijana wasio na nidhamu waliosajiliwa na kutumiwa kama nguvu ya chama tawala katika kila kijiji.

Wakati zimesalia wiki chache kabla ya uchaguzi wa rais na Bunge, mashirika hayo yanasema, kusimamishwa makundi hayo ni muhimu ili kuepusha machafuko katika kipinfdi cha uchaguzi na kuonyesha kwamba haki za binaadamu zinapaswa kuheshimiwa.

Idadi ya usajili umeongezeka kuelekea uchaguzi

Taarifa rasmi zinaashiria kwamba mpango huo ni mkubwa na usajili uliongezeka kwa kasi katika miezi ya kuelekea kwenye kampeni ya uchaguzi wa rais zilizoanza mwezi Novemba 2015.

Uganda Polizei in Kampala
Picha: picture-alliance/dpa/D. Kurokawa

Maafisa walisema polisi inalenga kuwa na kiasi ya watu 30 wa kundi hilo la wanaozuwia uhalifu katika kila kijiji, ikiwa na maana ya zaidi ya watu milioni moja kote nchini Uganda. Rais Yoweri Museveni na maafisa wengine wa ngazi ya juu wa serikali walipigwa picha mwaka jana wakiwa katika hafla kadhaa za kumaliza mafunzo kwa waliosajiliwa katika mpango huo , na wamekaririwa wakisema maelfu ya watu wamepewa mafunzo.

Mashirika ya haki za binaadamu ya Amnesty International na Human Rights Watch, yamewahoji wanachama 20 wa makundi hayo na zaidi ya 120 wenye uzoefu au walioathirika kutokana na vitendo vya kundi hilo kuanzia mwezi Mei hadi Desemba 2015, katika miji minane kote nchini Uganda. Kutokana na maelezo yao, kuna ushahidi wa kutosha kwamba mpango huo unaoitwa Wanaozuwia uhalifu haufuati sheria na unakipendelea chama tawala, kwa lengo la kuwanyanyasa wapinzani wa kisiasa na kupunguza uungaji mkono kwa wapinzani.

Mashirika ya haki za binaadamu yanasema kumeripotiwa visa vya watu kupigwa ngumi na virungu, kamatakamata hovyo na kuwapora fedha wanaokipinga chama tawala NRM na kusema waliofanya vitendo hivyo chini ya sheria ya Uganda, wanapaswa kushtakiwa kwa utesaji.

Chini ya sheria ya kimataifa inayohusika na haki za binaadamu, serikali ya Uganda inawajibika kuhusiana na visa hivyo kwa sababu watendaji wanayafanya hayo kwa niaba ya serikali na chama tawala.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman /Human Rights Watch Report

Mhariri:Iddi Ssessanga