1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Werder Bremen yatengana na kocha Skripnik

18 Septemba 2016

Klabu ya Bundesliga ya Werder Bremen imemfungashia virago kocha wake Viktor Skripnik wakati kocha Bruno Labadia wa SV Hamburg yuko katika mbinyo mkali baada ya kuanza vibaya katika msimu huu.

https://p.dw.com/p/1K4V8
Bundesliga Werder Bremen gegen Hertha BSC Berlin
Kocha wa zamani Werder Bremen Viktor SkripnikPicha: Franklin/Bongarts/Getty Images

Kumbukumbu za fahari na ushindi zinapotea kila baada ya kupita mwaka kwa Werder Bremen na SV Hamburg.

Vigogo hivyo kutoka upande wa kaskazini katika soka la Ujerumani vimeshinda mataji 10 ya ligi na vikombe tisa vya Ujerumani DFB Pokal baina yao. Timu zote mbili zinajivunia mataji ya Ulaya katika rafu zao. Pamoja na hayo misimu michache sana imeonesha ishara ndogo za kunyakua mataji mengine hivi karibuni.

Werder Bremen Trainer Viktor Skripnik
Kocha Skripnik kibarua kimeota nyasiPicha: picture-alliance/dpa/C. Jaspersen

Kipigo cha mabao 4-1 siku ya Jumamosi (17.09.2016) dhidi ya Borussia Moenchengladbach kilifikisha mwisho wa muda wa kocha Viktor Skripnik kuifunza timu hiyo, ambaye aliondoka katika klabu hiyo leo Jumapili(18.09.2016) na kikosi kizima cha benchi lake la ufundi baada ya timu kurejea katika uwanja wake wa nyumbani wa Weser leo Jumapili.

Skripnik sasa ni kocha wa tatu tangu kocha Thomas Schaaf ambaye alikaa katika timu hiyo kwa miaka 14 , na kuondoka Mei 2013.

Nako Hamburg kuna legalega

Kama ilivyo kwa Bremen , SV Hamburg imekuwa ikiyumba yumba na kufanya urafiki wa karibu na eneo la hatari la kushuka daraja, licha ya kuwa msimu uliopita ilifanikiwa kukaa katika nafasi ya kati ya msimamo wa ligi chini ya kocha Bruno Labbadia. Timu hiyo haijawahi kushuka daraja tangu kuingia katika daraja la kwanza la Bundesliga , lakini ubingwa wake wa mwisho katika Bundesliga ulikuwa mwaka 1983, mwaka ambao pia ilishinda kombe la ulaya.

Uongozi wa klabu na mabadiliko katika kikosi cha timu hiyo havikusaidia Hamburg kuweka mahesabu yao sawa ama kuleta mafanikio ya kimchezo. Klabu hiyo msimu uliopita ilikuwa na madeni yanayokadiriwa kufikia kiasi ya euro milioni 89, wakati ilipotangaza nakisi ya euro milioni 16.9 na kufanya hasara kwa miaka mitano mfululizo.

Deutschland Fußball Bundesliga Trainer Bruno Labbadia
Kocha wa Hamburg SV Bruno LabbadiaPicha: Getty Images/S. Hofmann

Hata hivyo , usemi wa mwisho haitoki kwa mkurugenzi wa spoti wa klabu hiyo katika klabu ambayo bilionea Klaus-Michael Kuehne alichangia zaidi ya euro milioni 30 kwa ajili ya kununulia wachezaji kabla ya msimu huu kuanza na atasubiri mafanikio ya uwekezaji wake.

"Tusubiri na kuona iwapo kocha Bruno Labbadia anaweza kuiweka timu hiyo katika hali nzuri," Kuehne alinukuliwa akisema kabla ya vipigo mfululizo dhidi ya Bayer Leverkusen na RB Leipzig.

Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae