1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Westerwelle ataka tahadhari Mashariki ya Kati

14 Juni 2011

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle, yuko ziarani Mashariki ya Kati, na ametaka hatua za tahadhari zichukuliwe katika kuutatua mgogoro wa Israel na Palestina.

https://p.dw.com/p/11ZtO
Waziri Mkuu wa Ujerumani, Guido Westerwelle, akiwa Benghazi
Waziri Mkuu wa Ujerumani, Guido Westerwelle, akiwa BenghaziPicha: picture alliance/dpa

Akiwa mjini Jerusalem hivi leo (14.06.2011), Westerwelle amesema kwamba jambo lililo wazi ni kuwa ni lazima mgogoro wa Mashariki ya Kati upatiwe ufumbuzi wa haraka na wa kudumu, lakini akatahadharisha kwamba uharaka huo usimaanishe kufanya mambo bila ya mashauriano.

Katika hali inayoonekana kama kwamba anazungumzia azma ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina kupeleka pendekezo la kutambuliwa kwa taifa la Palestina katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hapo Septemba, Westerwelle amesema kwamba kimsingi Ujerumani inaunga mkono kuwepo kwa taifa la Palestina, lakini lazima kupitie njia sahihi:

"Jambo moja liko wazi kwa sera ya nje ya Ujerumani: Tunataka papigwe hatua za kwenda mbele. Ni muhimu kwa usalama wa ndani wa Israel kuhakikishwa, lakini pia ni muhimu kuwa na taifa la Palestina. Yote mawili yanatakiwa kuzingatiwa na kupitia njia muafaka." Amesema Westerwelle katika mahojiano yake na Deutsche Welle.

Guido Westerwelle na Waziri wa Maendeleo wa Ujerumani, Dirk Niebel
Guido Westerwelle na Waziri wa Maendeleo wa Ujerumani, Dirk NiebelPicha: picture-alliance/dpa

Westerwelle amesema kwamba suala la mgogoro wa Palestina na Israel na wimbi la mageuzi katika ulimwengu wa Kiarabu hivi sasa ni mambo yanayokwenda sambamba na ni lazima kupatiwa suluhisho linalofaa.

Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Ujerumani amezitaka pande zote mbili za mgogoro huu kurudi mezani kwa mazungumzo ya kiadilifu na yenye dhamira ya kuutatua kikwelikweli mgogoro huu mkongwe wa Mashariki ya Kati.

Hata hivyo, Westerwelle amesema kwamba ni lazima pande zinazohusika kutokuzingatia tu maslahi ya siasa za ndani za mataifa yao.

Akionekana kuzungumzia msimamo mkali uliotolewa na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, katika hotuba zake za mwezi uliopita nchini Marekani, Westerwelle kwamba "Kwa kuwa na misimamo mikali, mtu anaweza kupata sifa kwenye siasa za ndani, lakini hilo halitatui tatizo lililopo."

Ziara hii ya Mashariki ya Kati ni muendelezo wa ziara ya jana nchini Libya, ambako akiwa pamoja na Waziri wa Maendeleo, Dirk Niebel, Westerwelle alikutana na Baraza la Mpito la Kitaifa linaloongozwa na waasi wa Libya, mjini Benghazi.

Hivi leo anatarajiwa kutembelea Wakfu wa Auguste Victoria mjini Jerusalem, kabla ya kuenda Ramallah, ambako atakutakana na waziri mkuu wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina, Salam Fayad. Jioni atarudi tena mjini Jerusalem ambako atakuwa na mazungumzo na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Nentanyahu, na Waziri mwenzake wa Mambo wa Nje, Avigdor Libermann.

Kwa upande wake, Waziri Niebel atatembelea miradi ya kimaendeleo inayofadhiliwa kwa ushirikiano wa Ujerumani na Palestina katika Ukanda wa Gaza.

Mwandishi: Mohammed Khelef/DPA
Mhariri: Othman Miraji