1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

charges against al -Bashir

Mtullya, Abdu Said15 Julai 2008

Jee rais wa Sudan al Bashir atafunguliwa mashtaka?

https://p.dw.com/p/Ed42
Rais Omar al-Bashir wa Sudan.Picha: AP

Hatua ya kumfungulia mashtaka rais Omar Al Bashir wa Sudan ambae bado yupo madarakani inatishia kuigawanya jumuiya ya kimataifa. Nchi za magharibi zinataka rais huyo ajibu mashtaka juu ya mauaji halaiki wakati Urusi na China zinapinga.Iwapo rais Omar al-Bashir atafikishwa mahakamani kujibu mashtaka hayo, hiyo itakuwa ni mara ya kwanza kwa kiongozi aliepo madarakani kufanyiwa hivyo.

Mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama ya kimataifa inayopamabna na uhalifu Luis Moreno Ocampo- ICC amewasilisha ushahidi kuthibitisha kuwa rais al- Bashir ametenda uhalifu wa mauaji halaiki katika jimbo la Darfur. Ushahidi huo ulifutia miaka mitatu baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kumpa jukumu la kuchunguza mashtaka. Kinachosubiriwa sasa ni kutolewa hati ya kisheria ili rais al- Bashir aweze kukamatwa.

Hatahivyo mwendesha mashtaka amewasilisha ombi kwa mahakimu 18 wanaowakilisha kanda takriban zote za dunia.

Wanaweza kukubali au kukataa ombi hilo.

Lakini utaratibu huo unaweza kuchukua miezi kadhaa kutokana na sababu za kisiasa hasa kwa kuzingatia kwamba al-Bashir ni mkuu wa nchi ya kiafrika.

Pia pana utata mwingine.

Chini ya ibara ya 16 ya mkataba wa Rome uliowezesha kuundwa mahakama ya kimataifa, ICC, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lina mamlaka ya kuzuia mashtaka yoyote dhidi ya rais wa Sudan kwa kipindi cha miezi 12. Baraza la Usalama linaweza kutoa ombi hilo kwa mara nyingine kwa kutumia hoja zilezile. Hakuna uchunguzi au mashtaka yanayoweza kufunguliwa ikiwa ibara hiyo ya 16 itatumiwa na Baraza la Usalama.

Mwakilishi mmoja wa kibalozi pia amesema, kuwa China na Urusi, zilizopinga vikwazo dhidi ya Zimbabwe wiki jana huenda zikaamua kutopiga kura ikiwa Marekani,Ufaransa na Uingereza zitatoa hakikisho kwamba Baraza la Usalama halitaunga mkono mashtaka dhidi ya rais al-Bashir.

Ikiwa mahakama ya kimataifa ICC itatoa hati ya kuwezesha kukamatwa kwa rais Omar al-Bashir ,hatua hiyo itakuwa na athari za kisiasa na kijeshi na hivyo itavuruga juhudi za amani zinazoendelea sasa nchini Sudan. Hatua ya mahakama ya kimataifa pia inaweza kuhatarisha usalama wa wanajeshi alfu 9 wa Umoja wa Mataifa na wa Umoja wa Afrika wanaolinda amani nchini Sudan.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ambae amepitisha juhudi kubwa za kuleta amani nchini Sudan amejiweka kando na maamuzi ya mahakama ya kimataifa na ya mwendesha mashtaka wake mkuu.


Baadhi ya watalamu wa sheria wanasema hatua ya mahakama ya kimataifa imekuja wakati mbaya. Mtaalamu mmoja amesema kuwa hakuna shaka kwamba rais al-Bashir anahusika na matukio ya Darfur, lakini mashtaka ya mahakama kuu ya kimataifa hayatasaidia katika juhudi za kuleta amani nchini Sudan.

Msimamo huo umesisitizwa pia na Umoja wa Afrika.Umoja huo umesema haki itendeke lakini bila ya kuzuia juhudi za amani.