1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wito kupiga marufuku chama cha NPD

P.Martin25 Agosti 2007

Polisi katika mji wa Mainz,nchini Ujerumani imemshtaki mwanaume wa miaka 29,baada ya Waafrika 2 kushambuliwa na wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia mwishoni mwa juma lililopita.

https://p.dw.com/p/CHja

Msudani mmoja alijeruhiwa vibaya na vile vile Mmisri alipata majeraha madogo baada ya kupigwa na chupa.Wenyeji waliingilia kati kuwasaidia wageni hao na wanaume 3 wamekamatwa.Shambulizi hilo lilitokea baada ya tamasha la mvinyo kwenye mji wa Guntersblum,katika jimbo la Rhineland Palatinate.

Vile vile siku hiyo ya Jumamosi katika jimbo la Saxony,mashariki ya Ujerumani,Wahindi 8 walipigwa na kundi la watu 50,ikidhaniwa kuwa waliohusika ni wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia.Baadhi ya Wahindi walioshambuliwa, walihitaji kupelekwa hospitali.

Mashambulizi haya ya ubaguzi yamechochea miito mipya ya kukipiga marufuku chama cha NPD cha Nazi-Mamboleo.

Kamisheni ya Ulaya imesema,itasaidia juhudi zo zote za serikali ya Ujerumani kukipiga marufuku chama cha NPD.Naibu Rais na Kamishna wa Sheria wa Halmashauri ya Ulaya,Franco Frattini ameliambia gazeti la Kijerumani,“Bild am Sonntag“ kuwa Ujerumani sawa na Ufaransa,Ubeligiji,Denmark na Italia inakabiliwa na tatizo kubwa la wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia.

Katika mwaka 2003,jeribio la kukipiga marufuku chama cha NPD halikuweza kufanikiwa.