1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Steinmeir airejeshea Hadhi yake Wizara ya Nje

28 Desemba 2015

Kuzidi hadhi wizara ya mambo ya nchi za nje ya Ujerumani, kilio cha jeshi la shirikisho na juhudi za kuwavunja nguvu wanamgambo wa IS ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa zaidi na wahariri magazetini

https://p.dw.com/p/1HURy
Waziri wa Mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier alipokuwa ziarani mjini Kampala Uganda Novemba 21 mwaka huuPicha: picture-alliance/B. Jutrczenka

Tuanzie lakini Berlin ambako wizara ya mambo ya nchi za nje inasemekana inazidi kujipatia umaarufu na sifa,miaka miwili tangu ilipoanza kuongozwa na mwanasiasa wa chama cha Social Democratic SPD,Frank-Walter Steinmeier. Gazeti la "Mannheimer Morgen" linaandika: "Tangu Frank-Walter Steinmeier alipokabidhiwa hatamu za uongozi,wizara hiyo imeanza upya kujipatia umuhimu na umaarufu mkubwa baada ya kujitoa chini ya kivuli cha wizara ya fedha. Imefika hadi mtu anaweza kuzungumzia kuhusu mapambazuko ya siasa ya nje ya Ujerumani. Na Ujerumani imeanza taratibu kugeuka dola kuu,ikibebeshwa majukumu ya uongozi,ingawa haimiliki silaha za kinuklea na wala si mwanachama wa kudumu wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa-haina tamaa ya kuwa dola lenye nguvu na ndio maana inasifiwa kuwa dalali muaminifu na mpatanishi wa kuaminika.

Jeshi la Shirikisho Bundeswehr liko Hali Taabani

Maoni sawa na hayo yametolewa pia na gazeti la Badische Neueste Nachrichten. Picha ya kuhuzunisha lakini inachorwa na wahariri wa magazeti kuhusiana na hali namna inayolikumba jeshi la Ujerumani Bundeswehr. Gazeti la "Stuttgarter Nachrichten"linazungumzia kilio cha shirika linalopigania masilahi ya wanajeshi wa Ujerumani na kuandika:"Likijikuta katika hali mbaya kabisa, jeshi la shirikisho-Bundeswehr limeanza kuporomoka tangu miaka 25 iliyopita. Kilio cha kuomba msaada kutoka Bundeswehr wanasiasa wanabidi wakizingatie kwa dhati. Shirikisho la vyama vinavyopigania masilahi ya wanajeshi linakadiria kwasasa kuna wanajeshi 20.000 wanaowajibika kwa njia moja au nyengine. Na sio tu nchi za nje. Wanajeshi 7000 wanashughulikia wakimbizi. Maneno mazuri yanayotolewa na waziri wa ulinzi pekee hayasaidii kitu. Anaetaka kuwajibika kimataifa anabidi awe na wanajeshi na zana zinazohitajika. Ndio maana kilio cha kupatiwa misaada kinabidi kiwagutuwe wanasiasa watambue"wanajeshi zaidi wanahitajika.

Gazeti la "Rhein-Neckar-"linahisi:"Badala ya kuidhinisha kwa pupa mipango ya kusajiliwa wanajeshi zaidi na kutolewa fedha zaidi,wanasiasa wanabidi waangalie kwa makini na kutambua majukumu ya aina gani hasa jeshi la shirikisho litakabiliana nalo siku za mbele na nini kitahitajika.

IS wanakaribia kuvunjwa Nguvu

Na mada yetu ya mwisho inahusiana na juhudi za kuwavunja nguvu wanamgambo wa itikadi kali wa dola la kiislam-IS. Gazeti la "Nordwest-Zeitung" linazungumzia mapingano ya kuukomboa mji wa Ramadi nchini Iraq na kuandika:"Hasha,bado hawajamalizika. Lakini wamepigwa vibaya sana. Jeshi la serikali ya Iraq linaonyesha kuukomboa mji wa mkoa wa Ramadi na katika eneo la kaskazini mwa Syria wanajihadi hao wamepokonywa pia bwawa muhimu la Tishrin. Kilichosalia ni kutaraji ngome za IS huko Mossul nchini Iraq na Rakka nazo pia zinakombolewa. Hapo tutaweza kuzungumzia kuhusu mwisho wa IS hata kama ugaidi wa itikadi kali bado utakuwa haujatokomea. Al Nusra na makundi mengineyo yanasubiri tu kukamata nafasi ya IS.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Mohammed Khelef