1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wizi wa nyaya za umeme, simu waongezeka Ujerumani

16 Julai 2012

Leo magazeti ya Ujerumani yanazungumzia kuogezeka kwa uhalifu wa wizi wa nyaya za umeme, mgogoro wa ndani wa kisiasa linapohusika suala la muelekeo wa serikali kwenye sarafu ya euro na sera ya nishati ya Ujerumani.

https://p.dw.com/p/15YIG
Nembo ya kampuni ya umeme na nishati ya RWE.
Nembo ya kampuni ya umeme na nishati ya RWE.Picha: DW

Gazeti la Mitteldeutsche Zeitung linazungumzia namna kiwango cha uhalifu kilivyopanda juu hapa Ujerumani. Kampuni ya Mawasiliano ya Telecom na ile ya umeme ya RWE zimekuwa zikishuhudia wizi mkubwa sana wa nyaya zake kwa siku za hivi karibuni.

Kwa mwaka uliopita, Telecom peke yake iliripoti matukio 3,800 ya wizi, ambapo jimbo la Saxony-Anhalt limeongoza. Wizi huo umeisababishia kampuni hiyo hasara ya euro milioni 20, ikiwa ni mara mbili zaidi ya hasara iliyopata mwaka 2010 kwa matukio kama hayo.

Gazeti hilo linataja kuwa sababu moja kubwa ya kuongezeka kwa wizi huo wa nyaya za umeme na simu, ni kupanda kwa thamani ya madini yanayotengezewa nyaya hizo, yaani shaba, ambapo sasa ni euro 4,500 kwa tani. Matokeo yake ni kuwa kila mwaka, kwa uchache, Telecom na kampuni ya umeme ya RWE hupoteza euro milioni 10.

Sigmar 'amkalia kooni' Merkel

Gazeti la Rheinische Post linazungumzia kauli kali kabisa kuwahi kutolewa na mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani cha Ujerumani, SPD, Sigmar Gabriel, kuhusiana na msimamo wa Kansela Angela Merkel kuelekea mfuko wa uokozi kwenye kanda ya euro, ESM.

Kiongozi wa chama cha SPD, Sigmar Gabriel.
Kiongozi wa chama cha SPD, Sigmar Gabriel.Picha: Reuters

Bila ya kutafuna maneno, Gabriel anasema kwamba sasa serikali ya mseto wa vyama vya CDU/CSU na FDP itachukua njia yake kivyake kuelekea euro, na isitaraji uungaji mkono wowote kutoka kwa wengine.

Kisa? Gazeti hilo linamnukuu Sigmar Gabriel wa SPD akitamka maneno haya: “Kiongozi wa mfuko wa ESM, Klaus Regling, amekiweka bayana kile Angela Merkel na viongozi wengine wanachokificha. Kwamba benki zinaweza kujitwalia mamilioni ya fedha za walipa kodi, baada ya kwamba zimeshayapoteza kwenye kamari, tena bila ya kulazimika kufanywa kwa mageuzi makubwa ya kisera katika nchi husika. Hii maana yake ni kuwa, walipa kodi wa Ujerumani, watabeba mzigo wa kulipa madeni ya benki za mataifa ya nje. Na ikiwa hilo ndilo CDU/CSU na FDP wanalolitaka, nawajue kuwa sio sisi!“

Rösler ataka mageuzi ya sheria ya nishati

Mwisho ni sera ya nishati ya Ujerumani, taifa ambalo licha ya kukusudia kuelekea moja kwa moja kwenye matumizi ya nishati salama, ukweli uliopo mbele yake ni mwengine. Rheinische Post linasema Waziri wa Uchumi wa Ujerumani, na ambaye pia ni mwenyekiti wa FDP, Phillip Rösler, anataka mageuzi makubwa katika Sheria ya Vyanzo vya Nishati Jadidifu, linasema gazeti hilo.

Waziri wa Uchumi wa Ujerumani, Phillip Rösler.
Waziri wa Uchumi wa Ujerumani, Phillip Rösler.Picha: Picture-Alliance/dpa

Rösler anasema kwamba sheria hiyo inapaswa kufanyiwa mageuzi makubwa ili raia na wafanyabiashara walipie umeme kwa bei rahisi, maana taifa haliwezi kubahatisha kukosa umeme wa uhakika na rahisi kama kweli linataka kubakia kwenye sifa ya kuwa taifa la kiviwanda.

Mwandishi: Mohammed Khelef
Vyanzo: Mitteldeutsche Zeitung/Rheinische Post
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman