1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wolfgang Clement, makamo wa zamani wa kiongozi wa chama cha SPD cha Ujerumani, afukuzwa chamani.

Othman, Miraji31 Julai 2008

Wolfgang Clement afukuzwa kutoka Chama cha SPD cha Ujerumani

https://p.dw.com/p/Enlw
Wolfgang Clement, waziri wa zamani wa uchumi wa UjerumaniPicha: AP

Waziri wa zamani wa uchumi wa Ujerumani, ambaye pia aliwahi kuwa waziri kiongozi wa mkoa wa North Rhein Westfalia, unaokaliwa na watu wengi kabisa hapa Ujerumani, Wolfgang Clement, amefukuzwa kutoka chama chake cha Social Democrati, SPD. Kwa mujibu wa televisheni ya hapa Ujerumani, ZDF, ni kwamba hatua hiyo imechukuliwa na tawi la SPD la mkoa huo kutokana na matamshi alioyatoa Bwana Clement kabla ya uchaguzi wa mkoa wa Hesse ambapo aliipinga siasa ya nishati ya mtetezi wa uwaziri kiongozi wa mkoa huo kwa tiketi ya Chama cha SPD, Bibi Andrea Ypsilanti.

Uamuzi huo umechukuliwa na tume ya upatanishi ya chama cha SPD katika mkoa wa North Rhein Westfalia anakotokea Bwana Clement. Na punde hivi tume hiyo imeitangaza rasmi hatua yake hiyo mjini Berlin. Bwana Clement amesababisha malalamiko mengi ndani ya chama chake pale kabla ya kufanyika uchaguzi wa mkoa wa Hesse, kichini chini alitoa mwito asichaguliwe mtetezi wa SPD, Bibi Andrea Ypsilanti, kwa wadhifa wa waziri kiongozi. Sababu alioitoa ni kwamba siasa za nishati za bibi huyo sio nzuri. Tume ya upatanishi ya SPD katika wilaya ya Bochum iliisikiliza kesi hiyo ambapo Bwana Clement alisema hakubaliani na hatua hiyo. Mwezi uliopita Bwana Clement alijitetea mbele ya tume ya upatanishi ya mkoa, na akasema kwamba ataendelea kupinga siasa za chama chake, licha ya kusisitiza kwamba anataka bado kubakia kuwa mwanachama wa SPD. Lakini wale waliotaka Wolfgang Clement afukuzwe kutoka SPD wanadai kwamba upinzani na kiburi cha mwanasiasa huyo kimekiumiza chama hicho, hasa wakati wa uchaguzi wa Mkoa wa Hesse. Na kimedai kwamba uamuzi kama huo unamfaa mtu yeyote aliyetenda jambo kama hilo. Lakini wakili wa Bwana Clement, ambaye ni waziri wa zamani wa sheria, Otto Schily, hapo kabla alisema atapanda ngazi zote za chama cha SPD kuubatilisha uamuzi huo. Mwenyewe Wolfgang Clement ameshtushwa na uamuzi huo. Nacho chama cha FDP, ambacho sasa kiko upande wa upinzani, kimesema kitakuwa tayari kumpokea kwa mikono miwili Bwana Clement kama mwanachama wake. Makamo wa mkuu wa Chama cha FDP, Rainer Brüderle, aliliambia gazeti la TAGESZEITUNG la Berlin kwamba Chama cha SPD kinajiharibia kwa namna kinavomtendea mwanasiasa wa heshima kama Wolfgang Clement.

Hata hivyo, huu sio mwisho wa mwanasiasa huyo aliyewahi kukamata nyadhifa muhimu hapa Ujerumani katika ngazi za serekali ya mkoa na ya shirikisho. Aliwahi pia kuwa makamo wa mkuu wa Chama cha SPD. Tume ya upatanishi ya taifa ya chama cha SPD inaweza ikaitishwa kusikiliza upya kesi hiyo. Mwenyewe Clement yuko likizo. Si siku nyingi zilizopita, alizusha kasheshe nyingine ndani ya chama chake pale aliposema kwamba kutokana na kupanda juu sana hivi sasa bei za mafuta na gesi ya ardhini, inafaa vinu vya kinyukliya vinavotoa nishati vikabakishwa kuweko kwa muda mrefu zaidi.

Kuna watu wengine wanaohisi umauzi huo wa SPD katika mkoa wa North Rhein Westfalia kumfukuza chamani Bwana Clement ni usiokuwa sawa; wanasema ingefaa mwanasiasa huyo akaripiwe kwa vile hajaonesha mashikamano na chama chake, lakini sio afukuzwe kutoka chama. Mkongwe wa chama cha SPD, Erhard Eppler, amesema mtu aliye na mawazo mengine na chama chake katika mambo yote muhimu, hafai kuwa mwanachama wa chama hicho.