1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wolfowitz akwepa maswali ya waandishi wa habari

Josephat Charo12 Aprili 2007

Rais wa benki ya dunia, Paul Wolfowitz, alikwepa maswali kuhusu mpenzi wake wa muda mrefu, Shaha Riza, kuongezewa mshahara mkubwa uliozusha manung´uniko miongoni mwa wafanyakazi wa benki hiyo. Kashfa hiyo inaendelea kushika kasi huku habari zaidi zikiendelea kufichuka. Josephat Charo anaarifu zaidi.

https://p.dw.com/p/CHlE
Rais wa benki ya dunia Paul Wolfowitz
Rais wa benki ya dunia Paul WolfowitzPicha: AP

Rais wa benki ya dunia, Paul Wolfowitz, jana alitokwa na kijasho chembamba wakati kashfa inayomhusu mpenzi wake mzaliwa wa Libya, Shaha Riza, ilipotishia kuvuruga mkutano wake na waandishi wa habari ambao ulihusu maswala ya Afrika. ´Mnatakiwa kuuliza maswali na mimi natakiwa kujibu,´ alianza kutetemeka bwana Wolfowitz alipoulizwa swali la kwanza kumhusu mpenzi wake Shaha Riza, ambaye alipokea karibu dola laki mbili wakati alipokuwa akifanya kazi ya nje katika wizara ya ulinzi ya Marekani.

Alipoulizwa kinachoendelea kuhusu kashfa inayomkabili Shaha Riza, bwana Wolfowitz alisema na hapa ninamnukulu, ´Tuna kamati maalumu inayoshughulikia swala hilo. Binafsi nimeridhika kwa hilo na hayo ndiyo ninayoweza kuyasema kwa sasa, ´ mwisho wa kumnukulu Paul Wolfowitz.

Alipoulizwa ikiwa yeye binafsi alihusika kubadili sheria ili kumpa kazi Riza, Wolfowitz alirudia maneno aliyoyasema na kukataa kutoa maelezo zaidi. Wolfowitz kwa hasira aliwakanya waandishi wa habari wasiulize maswali ambayo hayakuhusiana na mkutano aliokuwa ameuitisha kuhusu Afrika.

Imefichuka kwamba Shaha Riza ana historia ya kuvunja sheria za benki huku akinufaika kifedha kutokana na kazi zinazohusiana na cheo alichokuwa nacho mpenzi wake Paul Wolfowitz katika wizara ya ulinzi ya Marekani, Pentagon.

Kwa mujibu wa shirika la kupambana na ufisadi la Government Accountability Project, GAP, duru za ndani ya benki ya dunia zimedhihirisha kwamba pamoja na Shaha Riza kuongezewa mshahara mkubwa mara mbili katika miaka ya hivi karibuni, hakuwasilisha ombi lolote la kutaka kazi wala kupewa ruhusa ya kufanya kazi na kampuni kubwa ya ulinzi ya Marekani, SAIC, wakati Wolfowitz alipokuwa naibu waziri wa ulinzi.

Katika toleo lake la mwezi Machi gazeti la Vanity Fair liliripoti kwamba Shaha Riza alipokea mishahara kama mtaalamu wa Mashariki ya Kati wa kampuni ya SAIC wakati kampuni hiyo ilipokuwa ikitoa habari za ujasusi kwa wizara ya ulinzi ya Marekani, Pentagon, kabla uvamizi wa Irak mnamo tarehe 19 mwezi Machi mwaka wa 2003.

Shaha Riza alihamishwa kutoka kazi yake kama afisa wa mawasiliano wa benki kuu ya dunia na kupewa kazi kwenye wizara ya ulinzi ya Marekani, Pentagon, mnamo mwezi Septemba mwaka wa 2005, muda mfupi baada ya Paul Wolfowitz kuchukua hatamu za uongozi wa benki hiyo kuzuia mgongano wa masilahi ya kibinafsi.

Katika matamshi yake ya kwanza hadharani kuhusu kesi hiyo, Paul Wolfowitz alisema anabeba dhamana kamili kwa maamuzi aliyopitisha kuhusu Shaha Riza, lakini akasema hakufanya makosa kwani alifuata ushauri wa kamati ya maadili ya benki kuu ya dunia.

Kashfa hiyo imemtia aibu bwana Wolfowitz huku akijaribu kupambana na ufisadi katika benki kuu ya dunia. Inaugubika pia mkutano wa mwaka wa benki hiyo utakaofanyika mwishoni mwa juma hili mjini New York.