1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wolfsburg yaanza mazoezi licha ya kifo cha Malanda

12 Januari 2015

Kiasi ya mashabiki 1,000 wa klabu ya hapa Ujerumani ya Wolfsburg wametoa heshima zao za mwisho kwa kiungo Junior Malanda, aliyefariki dunia mwishoni mwa wiki katika ajali ya barabarani siku ya Jumamosi

https://p.dw.com/p/1EIwu
Trauer nach Malanda-Tod
Picha: picture-alliance/dpa/Steffen

Na wakati mashabiki wakimuaga chipukizi huyo mwenye umri wa miaka 20, wachezaji wenzake wamewasili Afrika Kusini kwa ajili ya kambi ya mazoezi. Baada ya siku moja ya kutafakari, uongozi wa klabu hiyo uliamua kuendelea na safari yao ya kwenda mjini Cape Town.

Kocha Dieter Hecking alitiririkwa na machozi katika kikao cha waandishi wa habari wakati akisema kifo cha Malanda kimewacha “shimo kubwa“. Kiasi ya mashabiki 1,000 wa klabu hiyo walifanya matembezi ili kuomboleza kifo chake katika uwanja wa Volkswagen Arena jana Jumapili, wakiwa na bango lililokuwa na ujumbe wa “Pumzika kwa Amani Junior”.

Na siyo klabu ya Wolfsburg inayoomboleza tu, bali risala za rambirambi zimetumwa kutoka kila pembe. Rouven Schröder ni mkurugenzi wa michezo katika klabu ya Werder Bremen

Kiungo huyo alikuwa katika kiti cha nyuma cha gari akisafiri kujiunga na wenzake katika uwanja wa ndege wa Braunschweig, wakati gari hilo lilipougonga mti kati ya Bielefeld na Hanover.

Malanda aliichezea Wolfsburg mechi 17 za Bundesiga, na kufunga magoli mawili tangu alipowasili kutokea klabu ya Ubelgiji ya Zulte Wagerem. Kiungo huyo, nahodha wa timu ya taifa ya Ubelgiji ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 21, alionekana kuwa nyota wa siku za usoni.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/reuters
Mhariri: Josephat Charo