1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wolfsburg yaiangusha Hoffenheim

Bruce Amani
13 Februari 2017

Hoffenheim ilijikwaa kwa kupewa kichapo cha mabao mawili kwa moja na Wolfsburg, wakati vilabu vyote sita vinavyowafukuza vinara wa Bundesliga Bayern Munich vilipoteza mechi zao mwishoni mwa wiki

https://p.dw.com/p/2XTfU
Bundesliga Wolfsburg Hoffenheim Didavi Tor
Picha: Getty Images/AFP/R. Hartmann

Daniel Didavi aliingia baada ya mapumziko na kuisaidia Wolfsburg kupata ushindi katika kipindi cha pili wakati Hoffenheim wakipewa kichapo chao cha pili msimu huu. Didavi "Kwanza kabisa, ilikuwa muhimu kuwa tulikuwa bado katika mchezo. Kipindi cha kwanza hakikuwakizuri, tunajua sote, na katika kipindi cha pili hatimaye tulionyesha sura nyingine, kama timu, pia tuliwapa mashabiki msisimko. Nadhani ilikuwa muhimu kuwa tulionyesha tunachoweza uwezo wetu"

Bayern ya Carlo Ancelotti, ndiyo timu pekee kati ya sita za kwanza iliyoshinda wikendi hii baada ya Arturo Vidal na Arjen Robben kutikisa nyavu katika dakika za mwisho na kuwapa ushindi wa 2-0 dhidi ya washika mkia Ingolstadt. Bayern sasa wameongeza pengo la uongozi wao kileleni hadi pointi saba. "Ilikuwa mechi ngumu dhidi ya mpinzani aliyejipanga vyema. Haikuwezekana kupigiana pasi lakini nadhani tumekuwa na mchezo mzuri, na kulikuwa na nafasi za kufunga ili kuwa kifua mbele. Bila shaka bahati pia ilichangia". Alisema nahodha wa Bayern Philip Lahm

Deutschland Bundesliga Ingolstadt - Bayern
Bayern sasa wamepanua ungozi wao na pointi 7Picha: Getty Images/AFP/C. Stache

Hoffenheim wanabakia katika nafasi ya tano, lakini nyuma yao kuna FC Cologne ambao pia waliangushwa jana. Freiburg, mabingwa wa ligi ya daraja ya pili msimu uliopita, sasa wako katika nafasi ya nane baada ya kuwachabanga nambari saba Cologne 2-1 Maximilian Philipp, ni kiungo wa Freiburg "Tulijua kuwa Cologne walikuwa na mechi katikati ya wiki hivyo walikuwa na uchovu, na ilionekana hadi mwisho. Hawangeweza kucheza kwa kasi waliyoonyesha dhidi yetu katika mchuano wa awali. Sisi tulisubiri nafasi zetu na mwishowe tukafunga 2-1" Siku ya Jumamosi, nambari mbili RB Leipzig walipewa kichapo kwa wiki ya pili mfululizo baada ya kufungwa 3-0 nyumbani dhidi ya Hamburg. Ushindi huo uliwasaidia Hamburg kujiondoa katika nafasi tatu za mkia.

Nambari tatu Eintracht Frankfurt walifungwa 3-0 na Bayer Leverkusen wakati mshambuliaji Javier Chicharito Hernandez alifunga mabao mawili safi sana na kumwondolea shinikizokocha Roger Schmidt kufuatia vichapo vya mfululizo. "Hicho ndio kitu kizuri kuhusu mpira. Unaposhinda mchezo inaonyesha mambo ni mazuri na usiposhinda inaonyesha mambo ni mbaya". Alisema Schmidt

Hertha Berlin walibakia nafasi ya sita baada ya kuangushwa 2-0 na Schalke. Nambari nne Borussia Dortmund, waliangushwa 2-1 na washika mkia Darmstadt.

Yellow wall kufungwa

Dortmund - Signal Iduna Park - Leere Südtribüne
Ukuta wa Njano utafungwa kwa mechi mojaPicha: picture-alliance/augenklick/firo Sportphoto/R. Ibing

Na kando na kichapo hicho, masaibu ya BVB yameendelea leo, baada ya klabu hiyo kukubali kuufunga upande wa kusini mwa uwanja wanakosimama mashabiki wakati wa mchuano wa Jumamosi ijayo dhidi ya Wolfsburg. Hii ni baada ya klabu hiyo kukubali vikwazo ilivyowekewa na shirikisho la kandanda Ujerumani – DFB kufuatia vurugu za mashabiki wakati wa mechi dhidi ya Leipzig.

Hivyo ina maana BVB watacheza vila ya kushangaliwa na mashabiki sugu wa klabu hiyo ambao husimama katika eneo hilo maarufu la Yellow Wall au Ukuta wa Njano. Eneo hilo lililoko nyuma ya goli lina nafasi ya kusimama mashabiki 25. Kocha Thomas Tuchel alilaani vurugu hizo akisema uwanja wa mpira unapaswa kuwa mahala salama kwa familia zote

BVB pia wametozwa faini ya euro 100,000 baada ya mabango kadhaa kubebwa na mashabiki yakiwa na ujumbe wa matusi na kejeli dhidi ya klabu ya Leipzig. Vikombe vya plastiki pia vilirushwa uwanjani.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri:Yusuf Saumu