1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Xavi: 'Aibu' La Liga haina teknolojia ya mstari wa goli

22 Aprili 2024

Kocha wa Barcelona Xavi Hernandez amekashifu ligi kuu ya Uhispania La Liga kwa kutotumia teknolojia ya mstari wa mabao baada ya timu yake kushindwa 3-2 Clasico na kuwaacha Real Madrid ukingoni mwa taji.

https://p.dw.com/p/4f43a
Kandanda- Barcelona
Kocha wa Barcelona, Xavi Hernandez, akasirishwa na usimamizi wa La Liga.Picha: Gerard Franco/ZUMA Wire/imago images

Xavi alikasirika baada ya Lamine Yamal kupiga shuti ambalo Barcelona walisema lilivuka mstari lakini halikukubaliwa hata baada ya kuandaliwa na teknolojia ya VAR.

Yamal alipiga shuti kwa ufundi kuelekea lango na kipa wa Real Madrid Andriy Lunin ambaye alilipangua, lakini huenda lilikuwa tayari limevuka kuvuka mstari.

"Ni aibu,” alisema Xavi, akilalamika kwamba teknolojia inayotumika katika mechi nyingine za kiwango cha juu ikiwemo Ligi Kuu ya England haipatikani kwenyeLa Liga.

"Ikiwa tunataka kuwa ligi bora zaidi ulimwenguni lazima tusonge mbele kwa maana hii, lazima uweke teknolojia."

Mlinda mlango wa Barcelona Marc-Andre ter Stegen alikubaliana na kocha wake.

"Ni aibu kwa soka, sina maneno," alisema mchezaji huyo wa kimataifa wa Ujerumani.

"Kuna pesa nyingi sana katika ulimwengu huu lakini iweje hakuna pesa kwa kile ambacho ni muhimu zaidi."

Bao la dakika za mwisho la Jude Bellingham liliwaacha mabingwa Barcelona kwa pointi 11 nyuma ya Real Madrid zikiwa zimesalia mechi sita.

 "Madrid wamekuwa na ligi isiyo ya kawaida, wamepoteza mchezo mmoja tu, wamekaribia kumaliza," alikiri Xavi.  

"Ninahisi kwa mchezo tuliocheza kwa kawaida tungeshinda, tulishindana vizuri sana, nadhani tulistahili pointi tatu."

Real Madrid yaendelea kutamba

Soka la Uhispania -LaLiga
Kocha wa Real Madrid Carlo Ancelotti akimpa maelezo mchezaji inicius Paixao de Oliveira Junior wakati ya mechi.Picha: Jose M. Fernandez/NurPhoto/IMAGO

Kocha wa Real Madrid Carlo Ancelotti alisema alifurahishwa na kikosi chake  baada ya kuifunga Manchester City kwa mikwaju ya penalti na kutinga nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa na kisha kuandikisha ushindi wa dakika za lala salama katika Clasico. 

"Ninajivunia sana, kwa sababu ilikuwa michezo miwili muhimu sana," alisema kocha huyo.

"Sasa tunapaswa kujiandaa kwa sehemu ya mwisho ya msimu, lakini tuko katika nafasi nzuri sana."