1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Xi akaribisha uwekezaji wa kigeni akiwa Davos

Yusra Buwayhid
17 Januari 2017

Katika Mkutano wa Kimataifa wa Uchumi mjini Davos, Uswisi, Rais wa China, Xi Jinping, amesema China inakaribisha uwekezaji wa kigeni. Na kaonya dhidi ya kuzuka kwa vita vya kibiashara kufuatia kauli ya Donald Trump.

https://p.dw.com/p/2VwgX
Davos Chinas Präsident Xi
Picha: Reuters/R. Sprich

Rais wa China, Xi Jinping, ameonya katika mkutano huo kuwa vita vipya vya kibiashara havitosaidia maslahi ya upande wowote, na kufuata sera ya kulinda viwanda vya nchi kutaleta mwisho mbaya.

"Kutafuta ulinzi wa soko la ndani ya nchi ni kama kujifungia mwenyewe katika chumba cha giza. Ingawa utakuwa unajilinda dhidi ya upepo na mvua vinavyoendelea nje, lakini pia utakuwa unajinyima mwanga na hewa. Hakuna mtu itakayeibuka mshindi katika vita vya biashara," amesema Xi Jinping.

Rais huyo wa China hakuitaja Marekani au rais wake mteule Donald Trump ambaye anatarajiwa kuapishwa rasmi kama rais wa Marekani siku ya Ijumaa, lakini Xi ameonekana akijaribu kuijibu kauli ya Trump inayopinga mikataba ya kimataifa ya biashara huru pamoja na mipango yake ya kutaka kuipinga China katika masuala ya biashara.

Miongoni mwa mambo saba aliyoyataja Trump katika mpango wake wa biashara kama rais mpya wa Marekani, matatu yanaihusu China. Rais huyo mteule wa chama cha Republican anapanga kuipinga China katika sera yake ya fedha, kushitaki migogoro ya biashara inayoihusu China katika Shirika la Biashara Duniani WTO pamoja na kuichukulia hatua iwapo haitasimamisha biashara zake zisizofuata haki.

Ni mara ya kwanza kwa kiongozi wa China - ambalo ni taifa la pili kwa ukubwa kiuchumi baada ya Marekani - kuhudhuria Mkutano wa Kimataifa wa Uchumi unaofanyika kila mwaka mjini Davos, Uswisi.

Weltwirtschaftsforum in Davos
World Economic Forum ni Mkutano wa Kimataifa wa UcumiPicha: World Economic Forum/Benedikt von Loebell

Na Jumanne baraza la mawaziri la China, tayari limepitisha hatua za kuufungua zaidi mlango wa biashara wa taifa hilo ili kukaribisha uwekezaje wa kigeni, ikiwa ni pamoja na kulegeza mipaka ya uwekezaji katika benki na taasisi nyingine za kifedha.

Hata hivyo hakuna maelezo zaidi yaliyotolewa au ratiba ya utekelezaji wa mabadiliko hayo. Mwishoni mwa mwaka mpangaji mkuu wa serikali alisema kuwa serikali itachukua hatua za kulegeza masharti ya uwekezaji wa kigeni katika baadhi ya sekta.

Hatua hizo zinakuja wakati Rais Xi Jinping akiwa anajaribu kuionyesha China kama kiongozi wa kupambana na sera ya kulinda viwanda vya nchi na mtetezi wa utandawazi duniani. Katika Mkutano huo wa Kiamataifa wa Uchumi unaofaynika mjini Davos Uswisi, Xi amesema China itaendelea kuweka wazi mlango wake wa biashara na haitoufunga.

Hadi ifikapo Ijumaa wanasiasa wapatao 3,000, wafanyabiashara, viongozi wa Umoja wa Mataifa, wasomi pamoja na wanaharakati wanapanga kujadili masuala ya kimataifa kama vile suala la kukosekana kwa usawa na maendeleo ya kiteknolojia ambayo yanasababisha kupungua kwa nafasi za ajira.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/rtre/dpae

Mhariri:Josephat Charo