1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Xi Jinping asafishiwa njia China

14 Novemba 2012

Rais mtarajiwa wa China na waziri mkuu wake walianza safari yao kuelekea hatamu iliyoratibiwa kwa ustadi siku ya Jumatano, baada ya chama tawala kuwapandisha vyeo kwa kuwateua katika baraza muhimu la utawala.

https://p.dw.com/p/16jF3
Makamu wa rais wa China Xi Jinping na naibu waziri mkuu Li Keqiang.
Makamu wa rais wa China Xi Jinping na naibu waziri mkuu Li Keqiang.Picha: Reuters

Shirika la habari la China Xhinhua limethibitisha kuwa makamu wa rais Xi Jinping na naibu waziri mkuu Li Keqiang walichaguliwa katika kamati kuu ya chama mwishoni mwa mkutano wa wiki nzima, matokeo ambayo yalitarajiwa.

Rais anayemaliza muda wake Hu Jintao alisema wakati akifunga mkutano wa 18 wa chama tawala, kuwa mkutano huo umechagua kamati kuu mpya na kuwarithisha viongozi wa zamani na damu changa. Mabadiliko ya uongozi yalijadiliwa kati ya wazee wa chama na viongozi wanaostaafu, waliyo na shauku ya kulinda nguvu zao kisiasa na maslahi ya kifamilia, licha ya ukweli kwamba maslahi hayo laazima yalindwe kupitia mchakato wa uchaguzi katika mkutano huo.

Wagombea 10 wanaowania nafasi saba za kamati ya uongozi ya chama tawala cha CPC.
Wagombea 10 wanaowania nafasi saba za kamati ya uongozi ya chama tawala cha CPC.Picha: Reuters

Wajumbe 2,270 waliyochujwa kwa umakini walipiga kura zao za siri katika ukumbi wa Cavernous mjini Beijing kuchagua kamati mpya ya wajumbe kamili 205 na wengine 170 au zaidi wasiyokuwa na haki za kupiga kura. Kamati ndiyo itakayochagua siku ya Alhamis, kamati ya utawala yenye dazeni mbili za wajumbe na kamati kuu, ambayo yenye nguvu zaidi, itakayokuwa na wajumbe saba, ikiwa ni pungufu kutoka wajumbe tisa wa sasa.

Ni matokeo yaliyokuwa yakitarajiwa

Xi alikuwa akitarajiwa kwa muda mrefu kuwa ndiye atakayerithi kutoka kwa Hu, kwanza kama kiongozi wa chama wakati wa mkutano huu, na baadaye kama rais bunge litakapokutana kwa mkutano wake wa kila mwaka mwezi Machi mwakani, na hivyo kukamilisha awamu ya pili ya makabidhiano madaraka yenye mpangilio mzuri kwa chama hicho tangu kichukue madaraka mwaka 1949. Xi pamoja na Li wana uhakika wa kuwepo katika kamati ya utawala. Mtu wa tatu ambaye anaonekana kuwa na uhakika wa kuingia katika kamati hiyo ni mfanyabiashara nguli Wang Qishan, lakini kama kiongozi wa mapambano ya chama dhidi ya rushwa, baada ya kuchaguliwa katika kamati kuu kusimamia nidhamu.

Suala moja ambalolitapata majibu siku ya Alhamis ni endapo Hu anaweza kuendela kuhodhi madaraka, kama atabakiza nafasi yake kama mwenyekiti wa kamati kuu ya kijeshi, ambayo ndiyo chombo kikuu cha maamuzi cha jeshi la watu milioni 2.3 nchini China. Mtangulizi wa Hu, Jiang Zemin aliachia nafasi hiyo miaka miwili baada ya kukabidhi uongozi wa chama kwa Hu mwaka 2002. Li ndiye mrithi mtarajiwa wa waziri mkuu Wen Jiabao na moja ya majukumu yake litakuwa kusimamia uchumi wa taifa hilo ambao ni wa pili wa ukubwa duniani hivi sasa.

Wajumbe wakihudhuria hafla ya ufungaji wa mkutano wa 18 wa chama cha CPC.
Wajumbe wakihudhuria hafla ya ufungaji wa mkutano wa 18 wa chama cha CPC.Picha: Reuters

Wengine walioingia katika kamati

Maafisa wengine nane waliyotizamiwa kuwa wajumbe wa kamati ya uongozi wamefanikiwa kuchaguliwa katika kamati kuu, akiwemo Wang Qisham, kwa mujibu wa Xinhua. Orodha hiyo pia inajumlisha mchumi aliyepata mafunzo nchini Korea Kaskazini Zhanga Dejiang, waziri anayehusika na idara ya uratibu ya chama, Li Yuanchao, Mwenyekiti wa chama wa jimbo la Tianjin Zhang Gaoli na mhafidhina Liu Yunshan, ambaye ameviweka vyombo vya habari nchini humo chini ya udhibiti wake. Kiongozi wa chama katika jimbo la Guangdong ambaye anapendelea mageuzi, Wang Yang, mwenyekiti wa chama katika jimbo la Shanghai, Yu Zhensheng na Liu Yangdong, ambaye ndiye mwanamke pekee katika wagombea, nao walichaguliwa kuingia katika kamati kuu.

Orodha ya mwisho ya wajumbe wa kamati ya uongozi haitajulikana hadi viongozi wapya wajitokeze katika hafla fupi katika ukumbi wa Carvenous siku ya Alhamis. Ingawa kamati kuu inateua wajumbe wa kamati ya kisiasa na kamati ya uongozi, vyanzo vimeliambia shirika la habari la Reuters kuwa matokeo yamekwisha amuliwa na wenye nguvu ndani ya chama.

Chama chakubali marekebisho ya katiba

Baada ya siku kadhaa za hotuba na ishara za umoja, mkutano huo unaofanyika kila baada ya miaka mitano uliipitisha ripoti ya rais Hu Jintao kuhusu hali ya taifa, na kuridhia marekebisho katika katiba ya chama hicho, na kuingiza nadharia ya Hu maendeleo endelevu na ya usawa. Aliwambia wajumbe kabla ya kufunga mkutano huo kuwa wakati umefika kuweka huru fikira zao na kutekeleza sera ya mageuzi. Ripoti ya Hu ilionya kuwa rushwa inatishia uhai wa chama na taifa kwa ujumla, lakini akaongeza kuwa chama laazima kiendelee kushika hatamu.

Rais wa China anayemaliza muda wake Hu Jintao.
Rais wa China anayemaliza muda wake Hu Jintao.Picha: REUTERS

Makabidhiano ya huko nyuma yalikuwa yakigikita katika kukisafisha chama, huku yakigubikwa na njama na umuagaji damu- ikiwemo uteuzi wa Jiang kama kiongozi wa chama baada ya usambaratishaji wa maandamano karibu na uwanja wa Tianmen mwaka 1989. Uwanja huo ulizungushwa na bendera nyekundu na kunninga kubwa zinazoonyesha filamu za propaganda kwa wiki nzima, huku ameneo mengine ya mji yakiwa chini ya ulinzi mkali.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/rtre
Mhariri: Saum Yusuf Ramadhan