1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yaliyoandikwa magazetini hii leo

Oummilkheir31 Oktoba 2006

Ziara ya waziri mkuu wa Poland nchini Ujerumani,kurejeshwa wanajeshi wa Ujerumani kutoka Bosnia Herzegovina na kuchafuliwa mazingira ndizo mada zilizohanikiza magazetini

https://p.dw.com/p/CHUZ

Gazeti la SÜDDEUTSCHE Zeitung linaandika ifuatavyo kuhusu mkutano kati ya kansela Merkel na waziri mkuu Kaczynski:

“Uhusiano kati ya mataifa haya mawili jirani ni shuwari zaidi kuliko vile unavyodhaniwa mara nyingi na pande hizi mbili.Hata hivyo ishara za nia njema zinasaidia pia.Angela Merkel amefanya werevu aliposema mvutano kuhusu mabomba ya gesi yanayopitia bahari ya mashariki utatuliwe kwa daraja ya ulaya.Shauri hilo linavutia zaidi kuliko vile Poland inavyofikiria,kwasababu hata kama Warsaw inapinga, ujenzi wa mabomba hayo utafanyika tuu.

Kansela kwa hivyo ametekeleza ahadi aliyotoa ya kushughulikia kwa dhati zaidi hofu za Poland na nchi za Baltik,kuliko alivyofanya mtangulizi wake,kansela wa zamani Gerhard Schröder.Kwa sasa angalao hali imekua shuwari na ziara ya waziri mkuu wa Poland imekua ya maana licha ya patashika za awali.Kilichosalia ni kwa madola haya mawili kuyashughulikia zaidi masuala ya ulaya ,tena kwa pamoja na sio kinyume chake-linahisi gazeti la mSÜDDEUTSCHE Zeitung.

Gazeti linalochapishwa Weimar-THÜRINGISCHE LANDESZEITUNG linahisi “Poland inasalia kua jirani mzito.Hata hofu zao zizingatiwe kwa namna gani,Angela Merkel awe na fasaha na busara ya aina gani ili kutilia maanani masilahi ya Poland katika ujenzi wa mabomba hayo ya gesi na kujumuishwa Umoja wa ulaya katika kujengwa kituo cha waliotimuliwa-mjini Warsaw,watu wanasalia pale pale.

Cha kutia moyo lakini ni uchunguzi wa maoni ya umma wa hivi karibuni unaoonyesha imani ya wapoland kwa wajerumani imeongezeka .Wajerumani wanaoitembelea Poland wanathibitisha habari hizo.Lakini ndugu wawili wa Kaczynski na wafuasi wao,hawajali hayo wao.”

Gazeti la WESTDEUTSCHE ALLGEMEINE la mjini Essen linaamini uchaguzi ungeitishwa hii leo nchini Poland,basi wafuasi hao wa siasa kali za kizalendo wangerejea kuvikalia viti vya upinzani bungeni.Wengi wa wananchi wa Poland wanataka ushirikiano wa dhati zaidi na umoja wa ulaya na wanaiangalia Ujerumani kama jirani mwema na muaminifu.Ulaya itafaidika zaidi uhusiano utakapokua mzuri kati ya Poland na Ujerumani sawa na ule wa kati ya Ujerumani na Ufaransa.

Mada ya pili magazetini inahusu azma ya wizara ya ulinzi ya serikali kuu ya Ujerumani ya kuanza kuwarejesha nyumbani kuanzia mwakani,wanajeshi wa Bundeswehr walioko Bosnia Herzegovina.

Gazeti la SCHWÄBISCHE ZEITUNG linahisi huo ni uamuzi wa maana.Gazeti linaandika:

„Ni uamuzi unaostahiki huo pale waziri Jung aliposema anapunguza inadadi ya wanajeshi wa Ujerumani nchini humo.Wanaweza kupelekwa kwengineko wanakohitajika.Na utaratibu mpya wa kijeshi unaweza pia kudhamini hali ya usalama katika Bosnia Herzegovina.Makundi madogo madogo ya wanajeshi watakua na ofisi zao katika miji na vijiji vya nchi hiyo.Wanatakiwa kuleta hali ya kuaminiana na kua macho pia.Pakichomoza chokochoko tuu wanajeshi zaidi wanaweza kuletwa kuwasaidia.

Mada ya mwisho inahusu mazingira.Gazeti la Frankfurter Rundschau linachambua utafiti uliochambuliwa na waziri mkuu wa Uengereza Tony Blair na mtaalam wa zamani wa benki kuu ya dunia Stern mjini London.Frankfurter Rundschau linaandika:

„Mabilioni ya hasara kwa uchumi wa dunia hali ya ujoto itakapoongezeka kwa pointi tano hadi ifikapo mwisho wa karne hii.Mengi yaliyosemwa na Stern si mepya lakini kipya ni jinsi kuchafuliwa mazingira kutakavyoathiri shughuli za kiuchumi ulimwenguni.Wamarekani na wachina,linasema gazeti la Frankfurter Rundschau wameshaonywa kwa hivyo hazwastahiki tena kupuuza usafi wa mazingira.