1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yaliyoandikwa na wahariri wa Ujerumani hii leo

Oummilkheir14 Desemba 2006

Rais wa shirikisho aingia midomoni na sigara kupigwa marufuku mikahawani ndizo mada kuu magazetini

https://p.dw.com/p/CHUC

Lawama dhidi ya rais wa shirikisho Horst Köhler na majimbo kutakiwa yaamue kama watu waendelee kuvuta sigara mikahawani na kwenye baa au la,ndizo mada zilizotangulizwa mbele na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo.

Rais wa shirikisho Horst Köhler akifikia nusu tuu ya mhula wake,ameshaanza kuzongwa na lawama ambazo hazijawahi kushuhudiwa humu nchini kutoka vyama ndugu vya CDU/CSU na SPD pia.Chanzo,amekataa kutia saini sheria kadhaa zilizopendekezwa na serikali ya muungano wa vyama vikuu.Lawama dhidi ya rais wa shirikisho zimehanikiza kwa namna ambayo serikali kuu ya shirikisho imelazimika kuingilia kati na kuwasihi watu wawe wastahamilivu.Wahariri wa magazeti ya ujerumani wana maoni tofauti kuhusu msimamo wa rais wa Shirikisho Horst Köhler.

Gazeti la STRAUBINGER TAGEBLATT linampa haki rais köhler na kuandika:

„Kwa kuamua,katika kipindi cha chini ya wiki mbili kuzuwia miswaada ya sheria ya serikali ya rangi nyeusi na nyekundu,Horst Köhler,aliyekula kiapo atailinda na kuihami sheria msingi,hajakiuka madaraka yake,ameonyesha moyo wa ujasiri kuwapita baadhi ya watangulizi wake,ambao waliidhinisha sheria ambazo, ama hazikuambata na katiba au kwa mfano katika suala la sheria za uhamiaji,hazikupitishwa kuambatana na katiba.Köhler lakini hakutaka kufuata njia hiyo.“

Gazeti la WIESBADENER KURIER linahisi:

„Kimsingi rais wa shirikisho hajakosea hata kidogo alipokataa kuidhinisha sheria za kubinafsishwa shughuli za usalama wa safari za ndege,sawa na alivyopinga kutia saini sheria za kukusanywa maelezo kuhusu wanunuzi.Makelele ya watunga sheria katika makundi ya vyama vinavyounda serikali kuu ya muungano yamelengwa kuficha, pengine uzembe tuu walioufanya katika kadhia zote mbili au pengine hata makosa yaliyofanyika kwa kutathmini vibaya

matokeo ya mageuzi ya mfumo wa shirikisho.Hata hivyo rais wa shirikisho,badala ya kugoma kutia saini,ingekua bora pengine angeshauri mahakama kuu ya katiba mjini Karlsruhe iingilie kati.

Gazeti la STUTTGARTER NACHRICHTEN linahofia lawama hizo zisije zikaleta madhara.Gazeti linaendelea kuandika:

„“Kansela anajua:lawama dhidi ya rais zimedhamiriwa kuipagaza serikali yake makosa ambayo kimsingi yamesababishwa na serikali iliyopita ya muungano wa nyekundu na kijani.Lakini Merkel anatambua hatari iliyoko.Kwasababu katika serikali ya muungano wa vyama vikuu,kila mmoja ameingiwa na wasi wasi.Pindi rais akiendelea na msimamo wake mkakamavu,mipango mengine pia ya serikali kuu inaweza kukwama.“

Gazeti la BADISCHEN NEUESTEN NACHRICHTEN la mjini Karlsruhe linahoji:

„Tokea hapo uamuzi wa mwisho kuhusu uwiano uliopo kati ya mswaada wa sheria na sheria msingi, ni jukumu la mahakama kuu ya katiba .Hakuna anaebisha.Lakini pia ni jukumu la rais wa shirikisho, kukataa kuweka saini yake anapokua na shaka shaka kuhusiana na mswaada wowote wa serikali.Kumshinikiza afuate msimamo mwengine,hakutakua na maana kwea yeyote,si korti kuu ya katiba na wala si kwa raia wa kawaida.

Mada nyengine magazetini inahusu sigara.Kuanzia hivi karibuni watu hawataruhusiwa kuvuta sigara katika ofisi za serikali kuu.Lakini serikali za majimbo zinashindwa kukubaliana nani ni ahakku wa kuamua kuhusu suala hilo.Kamisheni maalum inapangwa kuundwa kusaidia kuufumbua mzozo huo.