1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yaliyochambuliwa na wahariri wa Ujerumani leo

1 Agosti 2011

Uturuki ambako wakuu kadhaa wa kijeshi wamejiuzulu,janga la njaa katika pembe ya Afrika na hali nchini Libya ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo.

https://p.dw.com/p/127QK
Majenerali wa jeshi la Uturuki wanaagaPicha: AP

Tunaanzia lakini nchini Uturuki ambako baadhi ya wahariri wa Ujerumani wanahisi kujiuzulu majemedari ni sawa na kusalim amri wanajeshi mbele ya wanasiasa.Gazeti la "Badische Neueste Nachrichten linaandika:

Kitendo cha kujiuzulu majemedari kinaashiria hali ya kukata tamaa.Wanaitupia serikali nyadhifa zao na kuondoka,kwasababu wanahisi hawawezi kushinda katika mvutano wao pamoja na waziri mkuu Recep Tayyip Erdogan kuhusu madai ya kupandishwa vyeo wanajeshi.Kujiuzulu wanajeshi kwa wingi kama hivyo,katika nchi yoyote ile nyengine hali hiyo ingeangaliwa kama tukio la ajabu na dalili ya ugonvi kati ya uongozi wa kijeshi na ule wa kisiasa.Nchini Uturuki lakini kuondoka majemedari sio tu ni kiroja bali ni ufa usiokuwa na mfano.Miaka kama kumi hivi nyuma wanajeshi wangekuwa pengine wameshauangusha utawala habithi wa kiraia.Hii leo wao ndio wanaoyapa kisogo madaraka yao na kumfanya Erodoggan aondoke na ushindi mkubwa

Gazeti la Rhein-Zeitung linaandika:

Wanajeshi wanapopokonywa madaraka,kimsingi hatua hiyo humaanisha ushindi kwa demokrasia.Lakini nchini Uturuki hali ni kinyume na hiyo.Kwasababu huko wanajeshi wanaonyesha kusalim amri katika kinyang'anyiro cha kuania madaraka dhidi ya chama cha kihafidhina cha kiislam AKP kinachoongozwa na waziri mkuu Raccep Tayyip Erdogan.Pande zote mbili hakuna mpenda demokrasia yeyote aliyekuwa akiziamini,hata hivyo hali ya kuchunguzana ndio iliyobuni wezani ulioifanya Uturuki iaminike na kuleta pia hali ya utulivu kisiasa nchini humo.Hali hiyo ya usawa imetoweka tangu mwishoni mwa wiki.

Dossierbild Horn von Afrika Ostafrika Somalia Hungersnot Hungerskatastrophe Bild 1
Wasomali wanakimbia janga na njaa na kuelekea KenyaPicha: AP

Mada yetu ya pili magazetini inatufikisha Somalia ambako gazeti la Main-Post la mjini Würzburg linaandika:

Kutokana na kitisho cha umati wa watu kufariki,kwa njaa,Umoja wa mataifa unabidi utumie madaraka yake yote kuzuwia visa vya kikatili vya wanamgambo wa itikadi kali ya dini ya kiislam.Yeyote yule anaefuata malengo ya itikadi kali za kidini bila ya kuzingatia hali ya watu wanaosumbuliwa kwa njaa,anastahiki azuwiliwe na ikilazimika hata kwa kutumiliwa nguvu.

Royal Air Force Typhoon
Ndege ya kijeshi ya Uengereza-Typhoon ni miongoni mwa madege ya NATO yanayotupa mabomu nchini LibyaPicha: picture alliance/dpa

Mada yetu ya mwisho inatufikisha Libya ambako mhariri wa gazeti la "Hannoversche Allgemeine Zeitung" anajiuliza kama mkakati unaotumika utaleta tija.Gazeti linaendelea kuandika:

Mkakati unaoonyesha kugeuka vita hausaidii kitu.Na ufumbuzi wa kidiplomasia utakuwa wa aina gani?Na utasimamiwa na nani?Marekani,Ufaransa na Uengereza wanaobeba jukumu kubwa katika opereshini za NATO nchini humo,watabidi kuwaachia wengine wakamate mstari wa mbele.Jumuia ya nchi za kiarabu inabidi iwajibike zaidi katika kusaka ufumbuzi wa amani.Ujerumani pia inaweza kutoa mchango wa maana.Hakuna sio katika Umoja wa mataifa na wala si mjini Tripoli,aliyesahau kwamba Ujerumani haijaunga mkono azimio la baraza la Usalama kuhusu vita vya Libya.Msimamo huo wa Ujerumani wakati ule uliwafanya wengi wakunje uso,lakini hii leo,unaweza kuifungulia njia ya kupatanisha.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Abdul-Rahman, Mohammed