1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

YANGON:Mawasiliano ya mtandao wa Internet yakatizwa

28 Septemba 2007
https://p.dw.com/p/CBLz

Mawasiliano makuu ya mtandao wa internet nchini Myanmar yamekatizwa baada ya siku mbili za machafuko katika mji mkuu wa Yangon.

Afisa mmoja wa mawasiliano ya simu amesema kwamba hali hiyo imesababishwa na kuharibiwa waya zilizo chini ya maji.

Lakini waandamanaji wanasema, huenda serikali imehusika na kukatiza mawasiliano hayo ili kuzuia kupelekwa nje taarifa zaidi na picha za video zinazo onyesha operesheni ya vikosi vya serikali dhidi ya waandamanaji wanao ipinga serikali ya kijeshi.

Vyombo vya usalama nchini Myanmar pia vimezifunga nyumba kuu tano za watawa katika mji mkuu wa Yangoon na kutangaza amri kwamba maeneo hayo hayaruhusiwi kufikiwa kwa ajili ya kuzuia ghasia zaidi.

Hatua hiyo imefuatia baada ya radio ya taifa kutangaza kuwa watu tisa waliuwawa jana baada ya wanajeshi kufyatua risasi na kutumia gesi ya kutoa machozi ili kuwatawanya waandamanaji.

Balozi wa Australia nchini Myanmar ameeleza wasiwasi wake kwamba huenda idadi ya watu waliouwawa ikawa zaidi ya watu tisa.

Wakati huo huo Marekani imezuia mali za maafisa 14 wa Myanmar.