1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yanukovich aongoza uchaguzi Ukraine

8 Februari 2010

Kiongozi wa upinzani nchini Ukraine Viktor Yanukovich amedai kupata ushindi mwembamba katika uchaguzi mkuu wa urais nchini humo, na hivyo kuashiria kurejea tena kwa nchi hiyo katika ushirika na Urusi.

https://p.dw.com/p/LvU7
Kuiongozi wa upinzani nchini Ukraine Viktor YanukovychPicha: AP

Wakati ambapo karibu asilimia 90 ya kura zote zimekwishahesabiwa, maafisa wa tume ya uchaguzi wamesema Yanukovich anaongoza akiwa na asilimia 58.49 ya kura huku mpinzani wake Waziri Mkuu BibiYulia Tymoshenko akiwa na 45.86 asimilia ya kura.

Kambi ya Bibi Yulia Tymoshenko imelalamika kuwepo kwa hila, ambapo jana usiku ilitaka kufanyika upya kwa zoezi la uhesabuji kura.Kuna uwezekano kuwa huenda waziri mkuu huyo akayapinga mahakamani matokeo hayo.

Lakini matokeo rasmi yanaonesha kurejea tena kileleni kwa Yanukovich ambaye anatajwa kuwa kibaraka wa Urusi, ikiwa ni miaka mitano baada ya waandamanaji kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa urais ambapo alishinda , uchaguzi ambao unadaiwa kufanyiwa hila kubwa.

Ushindi wa Yanukovich huenda ukashuhudia nchi hiyo yenye wakaazi kiasi ya millioni 46, ikibadilisha uelekeo wake na kuionyooshea tena mkono wa udugu Urusi.

Wagombea wote wawili, yaani Yanukovich na Tymoshenko walidai kuwa watashirikiana kwa karibu na Ulaya, lakini bibi Yulia anaonekana kuegemea zaidi upande wa Magharibi.

Hata hivyo Bwana Yanukovich amesema matokeo hayo ya uchaguzi yanaonesha ni jinsi gani watu wanataka mabadiliko.

Ukraine / Janukowitsch / Stichwahl
Viktor Yanukovych akipungia wafuasi wakePicha: AP

´´Watu wanataka mabadiliko, nadhani kwa matokeo ya uchaguzi huu tumejaribu kupiga hatua katika kuiunganisha tena Ukraine, kitu ambacho kwangu ni muhimu na lazima kwetu sote wawili kwa majaaliwa ya nchi yetu´´

Uwezekano unaonekana kuwa mdogo kwa Yanukovich kuendelea na juhudi za nchi hiyo kutaka kujiunga na Umoja wa kujihami wa NATO, juhudi ambazo ziliikera sana Urusi.

Yanakovich mwenye umri wa miaka 59 na ambaye aliwahi kuwa Waziri Mkuu katika utawala wa kikoministi wa Rais Leonard Kuchman mwaka 2005, amemtaka Bibi Yulia kujiuzulu wadhifa wa uwaziri mkuu.Hata hivyo wapambe wa Waziri Mkuu huyo wamesema kuwa wamehesabu asilimia 85 ya kura na kwamba mgombea wao anaongoza kwa 0.8 asilimia ya kura.

Yeye mwenyewe akiyapinga matokeo ya awali yaliyotangazwa na tume ya uchaguzi ya uchaguzi alisema.

Ukraine Präsidentenwahl - Yulia Tymoshenko
Waziri Mkuu wa Ukraine Yulia TymoshenkoPicha: AP

´´Nawaomba wale ambao wananisikiliza hivi sasa, kupambana kwa kutumia njia zote za protokali, kwa kutumia taarifa zote za uchaguzi kwa kila kura, kwa sababu kila kura inaweza kuamua majaaliwa ya Ukraine´´

Iwapo matokeo ya uchaguzi huo yatabakia kama yalivyo,Yanukovich atakuwa rais wa kwanza tokea uhuru wa nchi hiyo mwaka 1991 bila ya kupata ushindi wa zaidi ya 50 asilimia ya kura, ijapokuwa chaguzi katika miaka 1990 mara zote hazikuwa huru na za haki.

Baadhi ya wachambuzi wa siasa za Ukraine wanasema kuwa kutokana na hali iliyojitokeza ni dhahiri huenda Bwana Yanukovich akahitaji kufikia makubaliano na Bibi Yulia, na kuongeza kuwa huenda kambi za wagombea hao wawili ziko katika majadiliano.

Wachambuzi hao wanasema huenda Bibi Yulia Tymoshenko akakubali kushindwa lakini kwa makubaliano kuwa aendelee na wadhifa wa uwaziri mkuu, na kusubiri kuwania tena urais katika uchaguzi ujayo.

Mwandishi:Aboubakary Liongo/Reuters

Mhariri:Mohamed Abdul-Rahman