1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yar'Adua apishwa kuwa rais mpya wa Nigeria.

Mohamed Dahman29 Mei 2007

Umaru Yar’Adua amekuwa Rais mpya wa Nigeria leo hii akirithi mizozo mbali mbali ikiandamana na mashaka juu ya uhalali wake mwenyewe kufuatia uchaguzi uliokuwa na dosari.

https://p.dw.com/p/CHDY
Rais mpya wa Nigeria Umaru Yar' Adua.
Rais mpya wa Nigeria Umaru Yar' Adua.Picha: AP

Akipuuza wito wa upinzani wa kutaka kurudiwa kwa uchaguzi huo Yar’Adua amelishwa kiapo na hakimu mkuu kwenye uwanja wa gwaride la kijeshi katika mji mkuu wa Abuja katika seherehe zilizojumuisha bendi za kijeshi,wacheza ngoma walioavalia skati za nyasi na waigizaji wa michezo ya kuigiza.

Katika kiapoa hicho amesema kama rais wa Jamhuri ya Shirikisho la Nigeria atatekeleza kazi zake kwa uwezo wake wote kwa uaminifu na kwa mujibu wa katiba.

Gavana huyo wa zamani wa jimbo la Katsina mwenye umri wa miaka 56 amejizolea ushindi mkubwa katika uchaguzi wa rais wa mwezi uliopia ulioelezewa kuwa sio wa kuaminika na waangalizi wa uchaguzi wa kimataifa kutokana na kuwa na udanganyifu wa kura wa kila mahala pamoja na ghasia za matumizi ya nguvu.

Marekani na Uingereza mtawala wa zamani wa ukoloni kwa Nigeria zimetuma wajumbe wa ngazi ya chini kwenye sherehe hizo na viongozi wachache tu wa Afrika wamehudhuria sherehe hizo.

Katika taifa lililosibiwa na mapinduzi ya kila mara Wanigeria wamekukaribisha kuapishwa huko,.Mkuu wa idhaa ya Kihausa ya Radio Deutsche Welle Aliyu Umaru anasema Wanigeria wanachukulia sherehe za kuapishwa na ukweli kwamba ni mara ya kwanza kabisa katika historia ya nchi kukabidhiana madaraka kwa serikali moja ya kiraia kwenda nyengine kuwa ni ishara ya maendeleo na kuendelea kwa demokrasia nchini na ndio maana leo tarehe 29 mwezi wa Mei imetangazwa kuwa ni siku ya Demokrasia nchini Nigeria.

Yar’Adua mhadhiri wa zamani wa Kemia ameahidi kuendeleza mageuzi ya kiuchumi ya mtangulizi wake Olesegun Obasanjo ambayo yamempatia sifa ya kimataifa lakini yameshindwa kuwatowa kwenye dimbwi la umaskini wananchi wengi wa nchi hiyo.

Wakati akishika hatamu za madaraka Yar’Adua lazima apambane na umwagaji damu unaozidi kuongezeka katika jimbo la Delta linalozalisha mafuta ambao umekuwa ukitibuwa usafirishaji wa mafuta ghafi nje ya nchi ulio uhai wa uchumi wa taifa hilo pamoja na tishio la mgomo kutokana na kupanda ghafla kwa bei ya mafuta.

Lakini pengine mtihani mkubwa au changamoto kubwa zaidi itakuwa juu ya namna ya kumshughulikia Obasanjo ambaye ndie aliemtowa Yar’Adua kutoka asikojulikana miezi sita iliopita na kumfanya kuwa rais na ambaye hivi sasa anaonekana kuwa ameazimia kumuonyesha kuwa nani ni mkuu.

Katika siku za mwisho za utawala wake Obasanjo amepamdisha bei ya mafuta kwa asilimia 15,ameongeza maradufu ongezeko la thamani ya kodi na kuuza mitambo miwili ya kusafishia mafuta kwa washirika wake.

Kadhalika amefanya maamuzi kadhaa nyeti ambayo yangelipaswa kuachiliwa serikali mpya kama vile kufanya mabadiliko kwa safu ya juu jeshini na kuteuwa viongozi wa bunge wa taifa.