1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi yataka kuitumbukiza Yemen katika machafuko

22 Machi 2015

Rais wa Yemen amesema mashambulizi yaliouwa watu 142 katika misikiti ya Wahouthi yamekusudia kuitumbukiza nchi kwenye machafuko,umwagaji damu na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.

https://p.dw.com/p/1Eux3
Manusura katika msikiti mmojawapo ulioshambuliwa Sanaa. (21.03.2015)
Manusura katika msikiti mmojawapo ulioshambuliwa Sanaa. (21.03.2015)Picha: Reuters/Khaled Abdullah

Rais Abedrabbo Mansour Hadi aliyekimbia kutoka kifungo cha nyumbani katika mji mkuu wa Sanaa unaodhibitiwa na Wahouthi na kujihifadhi katika mji wa Aden ulioko kusini mwa nchi hiyo mwezi uliopita,amelaani mashambulizi hayo kuwa ni ya kigaidi,uhalifu na woga.

Katika baruwa kwa familia za wahanga na watu waliojeruhiwa 351 iliyotolewa na ofisi ya rais huyo Ijumaa usiku imesema mashambulizi hayo ya kinyama yanaweza tu kufanywa na maadui wa uhai ambao wanataka kuitumbukiza Yemen kwenye machafuko, umwagaji damu na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.

Hadi ameandika katika baruwa hiyo kwamba Washia wa itikadi kali wanaowakilishwa na wanamgambo wa Kihouthi na Wasunni wa itikadi kali wanaowakilishwa na kundi la Al-Qaeda ni sehemu mbili zilioko kwenye sarafu moja ambazo haziitakii mema na utengamno Yemen na watu wake.

Miripuko ya maafa

Miripuko kadhaa ya mabomu ya kujitowa muhanga yaliodaiwa kufanywa na kundi la Dola la Kiislamu imeuwa takriban watu 142 hapo Ijumaa katika misikiti ya Washia katika mji mkuu wa Yemen, Sanaa ikiwa ni mojawapo ya mashambulizi ya maafa makubwa kuwahi kufanywa na majihadi wa kundi hilo.

Rais Abd Rabbo Mansur Hadi wa Yemen.
Rais Abd Rabbo Mansur Hadi wa Yemen.Picha: picture-alliance/dpa/AP Photo//H.Mohammed

Mashambulizi hayo ni ya kwanza kudaiwa kufanywa na kundi la Dola la Kiislamu nchini Yemen na yanaonyesha nguvu kubwa iliokuwa nayo kundi hilo katika nchi ambayo kundi hasimu la Al Qaeda ndio mashuhuri kabisa miongoni mwa makundi wa wapiganaji wa jihadi ambalo limekanusha kuhusika na mauaji hayo kwa kusema kwamba mikakati yake sio kushambulia misikiti.

Waumini waliwakimbiza hospitali majeruhi kwa kutumia malori wakati watu wengine wakiondowa miili iliyokatika vipande vipande.Mshambuliaji mmoja wa kujitowa muhanga aliulenga msikiti wa Badr kusini mwa Sanaa wakati mshambuliaji mwengine aliwashambulia waumini waliokuwa wakikimbia nje kutoka msikiti huo.

Mshambuliaji wa tatu aliulenga msikiti wa Al-Hashush kaskzini mwa Sanaa wakati mshambuliaji wa nne alijiripuwa nje ya msikiti huo ambao hivi sasa unadhibitiwa na Wahouthi.Imam wa msikiti wa Badr alikuwa miongoni mwa watu waliouwawa. Duru zinasema mshambuliaji mwengine alijiripua nje ya msikiti katika ngome kuu ya Wahouthi ilioko katika mji wa Saada kaskazini mwa Yemen baada ya kushindwa kuingia ndani ya msikiti kutokana na usalama mkali. Mshambuliaji huyo alikuwa ni mtu pekee aliyepoteza maisha yake.

Mashambulizi ni mwanzo tu

Kwa mujibu wa Televisheni ya Wahouthi hospitali zilikuwa zinatowa wito kwa watu kuchangia damu.Katika taarifa iliyotolewa kwenye mtandao tawi la kundi la Dola la Kiislamu mjini Sanaa limesema mashambulizi hayo ni "mwanzo tu".

Wanajeshi na wanamgambo wafuasi wa Rais Hadi karibu na uwanja wa ndege wa Aden.(19.03.2015)
Wanajeshi na wanamgambo wafuasi wa Rais Hadi karibu na uwanja wa ndege wa Aden.(19.03.2015)Picha: AFP/(Getty Images

Taarifa imesema Makafiri wa Kihouthi wanapaswa kujuwa kwamba wanajeshi wa Dola la Kiislamu hawatopumuwa hadi hapo watakapowatokomeza Wahouthi na kuukata mkono wa Iran kwa mpango wake ilio nao kwa Yemen.Wahothi wanatuhumiwa kupatiwa msaada na Iran.Mashambulizi hayo ya Ijumaa yamekuja siku moja baada ya mapambano kati ya vikosi tiifu kwa Rais Hadi na vile vinavyowaunga mkono Wahouthi katika mji wa kusini wa Aden.

Tokea kukimbilia Aden mwezi uliopita,Hadi amekuwa akihangaika kuimarisha madaraka yake na hapo Alhamisi kiongozi huyo ilibidi aondolewe kwenye kasri la rais mjini Aden baada ya ndege ya kivita kufanya mashambulizi na kuuripua mlima ulioko karibu na kasri hilo.

Katika shambulio jengine tafauti hapo Alhamisi watu 11 waliuwawa wakati wapiganaji wa vikosi maalum tiifu kwa Wahouthi walipojaribu kuuteka uwanja wa ndege wa kimataifa wa Aden kutoka kwa wanamgambo walio tiifu kwa Hadi mapigano ambayo yalipelekea kufungwa kwa uwanja wa ndege huo.Hata hivyo uwanja wa ndege huo umefunguliwa tena Ijumaa.

Wahouthi wanyatia maeneo ya kusini

Kufuatia Wahouthi kuuteka mji mkuu wa Sanaa,Saudi Arabia na nchi nyengine za Ghuba zimehamishia ofisi zao za ubalozi mjini Aden na balozi kadhaa za mataifa ya magharibi zimefunga balozi zao katika mji mkuu wa nchi hiyo kwa sababu za usalama.

Mpiganaji wa kundi la waasi la Wahouthi nchini Yemen.
Mpiganaji wa kundi la waasi la Wahouthi nchini Yemen.Picha: M. Huwais/AFP/Getty Images

Tokea Wahouthi walipoudhibiti mji wa Sanaa hapo mwezi wa Septemba wamekuwa wakizidi kuimarisha hatamu zao madarakani katika vituo vya serikali wakisaidiwa na vikosi vilio tiifu kwa Rais wa zamani wa Yemen Ali Abdullah Saleh.

Lakini harakati zao za kutaka kudhibiti maeneo ya kusini zimekuwa zikikabiliwa na upinzani mkali wa vikosi vya kikabila vya Wasunni vyenye mafungamano na wanamgambo wa Al Qaeda ambao bado wana nguvu nchini Yemen.Kutokana Wahouthi kuendelea kuudhibiti mji mkuu wa Sanaa, Hadi ameutangaza Aden kuwa mji mkuu wa muda nchini Yemen.

Mwandishi : Mohamed Dahman/ AFP/AP

Mhariri : Caro Robi