1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yeyote atakayeshinda uchaguzi wa rais Marekani atalazimika kutathimini upya kuweko kwa majeshi Irak.

Abdulrahman, Mohamed18 Aprili 2008

Wachambuzi wanasema mzigo wa gharama unazidi kuwa mkubwa mno.

https://p.dw.com/p/DkE9
Wanajeshi wa Marekani wakiwa kwenye mapambano Irak.Picha: AP

Wagombea urais wa chama cha Democratic nchini Marekani Hillary Clinton na Barack Obama wanasema wanataka kuyaondoa majeshi ya Marekani nchini Irak haraka iwezekanvyo. Lakini mrepublican John Mcain anasema atayabakisha kwa kadiri inavyohitajika na amewahi kutamka kwamba hata kwa miaka mia moja.

Mchambuzi mmoja anasema kwamba wanasiasa wote hao watatu kwa hakika wanafahamu fika kwamba mzigo wa kugharimia vita vya Irak ni mkubwa na unauathiri uchumi wa Marekani, kwa hivyo ni wazi wanaufahamu ukweli wa mambo ulivyo na hatimae huenda wasiwe na chaguo jengine zaidi ya kufikiria kuwarudisha nyumbani wanajeshi ,kwa yeyote yule atakayefanikiwa kuingia madarakani hapo Novemba.

Mtaalamu wa siasa za Mashariki ya kati katika chuo kikuu cha Exeter nchini Uingereza Profesa Gerd Nonneman, anasema pia kwamba wenye wasi wasi na kutishwa zaidi ni viongozi wa Irak wanaoungwa mkono na Marekani, ambao wanahisi kuondoka mapema kwa wanajeshi wa kimarekani Irak kutawaadhiri kisiasa, lakini pamoja na hayo wanasema hawana wasi wasi na Mdemocrat kuingia Ikulu.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Irak Hoshiyar Zebari alinukuliwa na shirika la habari la Reuters akisema,"kwa yeyote atakayeingia Ikulu, kutakuweko na tathimini ya hali ilivyo na mabadiliko, lakini sio mapinduzi au kuondoka kabisa na kujitoa na kile kilichoekezwa Irak."

Kwa hakika idadi ya wanajeshi wa kimarekani nchini Irak tayari inapungua na haielekei kama hali itarejea kuwa sawa na ile ya mwaka jana, palipohitajika wanajeshi wa ziada . Hivi sasa kuna wanajeshi 160.000 nchini Irak , idadi ambayo itapungua hadi 140.000 ifikapo Julai pale brigedi 20 za mapambano,zitakaporudi nyumbani. Kamanda mkuu wa majeshi huko Irak Jenerali David Petraeus amesema ataanza tu kufikiria kupunguzwa kwa iadadi zaidi ya wanajeshi mwezi Septemba.

Hata baada ya wanajeshi hao kurudi nyumbani lakini, bado kutakuweko na brigedi 15 nchini Irak pamoja na mbili hadi tatu nchini Afghanistan

Wataalamu wanasema ili kuweza kutoa mafunzo ya ziada kwa wanajeshi awake, Mareakani itahitaji kupunguza iadadi ya vikosi hadi kufikia karibu 12.h Hiyo itakua na maana ya kuwa na wanajeshi watakaotoa msaada tu kwa wanajeshi wa Irak kwa mfano wa hujuma za anga , pale wanapokua katika mapigano na sio kuhusika katika upigaji doria wa kila siku.

Nusu ya majimbo 18 ya Irak yameshakabidhiwa wanajeshi wa Irak kusimamia shughuli za ulinzi yakiwemo maeneo ya washia upande wa kusini na ya wakurdi upande wa kaskazini.Makamanda pia wanasema wanashinikiza kukabidhi mamlaka ya maeneo ya Wasunni pia ambako wanajeshi wa Marekani wamo katika harakati za kupambana na wapiganaji.

Mkuu wa majeshi ya Marekani mjini Baghdad amesema juma hili kwamba makamanda wanamatumaini ya kukabidhi pia hatamu za ulinzi wa mji mkuu Baghdad kwa wanajeshi wa Irak katika muda wa karibu mwaka mmoja.

Chini ya zingatio la haya yote, wadadisi wanasema suali sio itachukua muda gani kwa yeyote atakayeingia madarakani kama rais wa Marekani baada ya rais George W.Bush kuwaondoa wanajeshi wa nchi hiyo nchini Irak , bali hali inadhihirisha kwamba atalazimika kufanya hivyo- awe ni Hilary Clinton, Barack Obama au John Mcain. Marekani inalazimika kutumia mamilioni ya dola kwa siku kugharimia mzigo huo wa vita sio tu Irak bali pia nchini Afghanistan na athari zake zimeanza kuuguza uchumi wa nchi hiyo.

Huenda wanajeshi walioko Irak wasirudishwe mara moja, lakini wachambuzi wanasema alau kutakuweko na ratiba ya kuondoka kwao, hali ambayo itawapa changa moto wanasiasa wa Irak kuchukua hatua madhubuti za kisiasa za kuwajibika na kuwa tayari kubeba mzigo wa mustakbali wao wa nchi yao , wao wenyewe. Uchaguzi wa rais wa Marekani utaafanyika mwezi Nobemba na rais mpya atashika rasmi madaraka Januari mwaka ujao.