1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zaidi ya 20 wauawa Somalia

18 Juni 2009

Zaidi ya watu 20 wameuawa Somalia katika mapigano ya usiku kucha kati ya wapiganaji wa kiislamu na wanajeshi wa serikali.Msikiti mmoja ulioko eneo la kaskazini mjini Mogadishu ulishambuliwa kwa bomu hapo jana

https://p.dw.com/p/ISjn
Wapiganaji wa Kiislamu mjini MogadishuPicha: AP


Wakati huohuo Waziri wa Ulinzi wa Somalia amenusurika baada ya shambulio la kujitoa muhanga kutokea katika hoteli aliyokuwamo.Mapema hapo jana mkuu wa polisi wa Mogadishu aliuawa pale wanajeshi wa serikali walipokuwa wakipambana na wanamgambo hao.


Mapigano hayo ya usiku kucha yametokea katika eneo la kusini na kaskazini mwa mji wa Mogadishu ambako wapiganaji wa makundi ya al-Shabaab na Hizbul Islam wako katika harakati za kumng'oa madarakani Rais Sheikh Sharif Sheikh Ahmed.Vita hivyo vilitokea pale wanajeshi wa serikali walipokuwa wakizishambulia ngome za wapiganaji wa kiislamu.Duru za polisi zinaeleza kuwa wanajeshi watatu waliuawa katika mapigano hayo nao raia 9 wa kawaida waliokuwa kwenye mtaa jirani wameuawa pia wakiwemo watoto watano kati yao.


Kulingana na mwandishi wa Shirika la Habari la AFP aliyeshuhudia tukio hilo maiti za watoto hao zilionekana kwenye kibaraza ambako walikuwa wanajaribu kujikinga milipuko ilipoaanza.Wote watano walifariki papo hapo baada ya kombora kulipuka walipokuwa wakijificha.

Dereva mmoja wa gari la kuwahudumia wagonjwa alisema kuwa kiasi cha watu 50 wamejeruhiwa katika mapigano hayo mapya.Naibu mkurugenzi wa hospitali ya Medina Dahir Dhere aliyezungumza na Shirika la Habari la Ujerumani DPA zaidi ya watu 10 walifikishwa katika hospitali hiyo kwa matibabu baadhi wakiwa na majeraha mabaya.

Taarifa za hivi punde zinaeleza kuwa Waziri wa Ulinzi wa Somalia amenusurika baada ya shambulio la bomu la kujitoa mhanga kutokea kwenye hoteli aliyokuwamo iliyoko katikati ya mji wa Baladwayne.Kulingana na afisa mmoja wa serikali aliyezungumza na shirika la habari la Reuters Waziri Omar Hashi Aden alishambuliwa alipokuwa katika eneo la Hiran.

Somalia Stadt Mogadishu
Mji wa Mogadishu uliogubikwa na mapiganoPicha: AP

Katika mashambulio ya mapema yaliyotokea hapo jana mkuu wa polisi wa mji wa Mogadishu Kanali Ali Said Hassan aliuawa pale wanajeshi wa serikali walipozishambulia ngome za wanamgambo katika wilaya iliyo eneo la kusini la Hodan.

Makundi ya wapiganaji wa kiislamu walianzisha operesheni ya kuusambaratisha utawala unaoyumbayumba wa rais Shariff Sheikh Ahmed tangu mwanzoni mwa mwezi wa Mei mwaka huu.Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa zaidi ya watu 122,000 wameachwa bila makazi tangu ghasia hizo kuanza na kuifikisha idadi ya wakimbizi wote nchini humo hadi milioni 1.3.Peter Smerdon msemaji wa Shrika la WFP tawi la Kenya anaeleza kuwa hali halisi ni mbaya

''Hali ni mbaya ni hilo linatuwia vigumu tunapojaribu kupeleka misaada wakati ambapo vita vinaendelea kwasababu watu wengi wanayakimbia makazi yao.Ni rahisi sana kwa wapiganaji kukiiba chakula kilichohifadhiwa kwenye magunia ndio mana tumesitisha ugawaji wa vyakula hivyo na badala yake tunawapa chakula kilichopikwa ambacho mtu anakila kisha anaondoka zake.''

Hali hiyo mbaya ya Somalia imewasababishia wakimbimbizi wa ndani kuzongwa na ukosefu wa bidhaa za matumizi ya kila siku kama makazi,maji na chakula.Kauli hiyo imetolewa na wawakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Watoto UNICEF lililokuwa na kituo kikubwa zaidi mjini Jowhar.Kituo hicho kilishambuliwa na wanamgambo yapata mwezi mmoja uliopita walioziiba bidhaa za matumizi zilizohifadhiwa.Katika taarifa yake iliyotolewa hapo jana na kaimu mkurugenzi wa shirika hilo Hannan Sulieman,maisha ya wanawake na watoto yako hatarini kwasababu ya wimbi jipya la ghasia linaloathiri shughuli za kutoa misaada ya kibinadamu.

Somalia imekuwa bila serikali imara tangu mwaka 1991 baada ya Rais Siad Barre kung'olewa madarakani.


Uteuzi wa rais Sheikh Sharif aliyekuwa mpiganaji wa kiislamu uliaminiwa kuwa ungechangia katika harakati za kusaka amani Somalia.Kwa upande wao wanamgambo wanahisi kuwa Rais Sheikh Sharif anaegemea zaidi upande wa mataifa ya magharibi.Osman Abokor ni mbunge wa chama cha Hanoolaato( chama cha kitaifa cha Somalia) na anaeleza kuwa kutowashirikisha wapinzani ndiko kulikosababisha hali iliyopo''Tunaweza kuwalaumu walioiteua serikali hii iliyoko bila ya ridhaa ya vyama vya upinzani vya Somalia.Tulimpendekezea mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Somalia Ahmed Ould Abdala kutochukua hatua hiyo kabla ya makundi ya al- Shabaab na Hizbul Islam hawajaondolewa serikali.Suala la msingi ni jee Umoja wa Afrika utaweza kuilinda serikali iliyopo?''


Kwengineko wanamgambo wanaripotiwa kuwashambulia wanajeshi wa serikali pamoja na vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Afrika AMISOM katika eneo la Bakara walipokuwa safarini kwenye barabara wanayoitumia mara kwa mara.


Mwaka 2007 wanamgambo walianzisha harakati zao punde baada ya wanajeshi wa Ethiopia walipoingia Somalia ili kuwafurusha wapiganaji wa mahakama za Kiislamu kundi lililokuwa likiongozwa na Sheikh Sharif na baadhi ya wanamgambo wengine.Kiasi cha raia alfu 18 wa kawaida wamepoteza maisha yao kwasababu ya uasi unaoendelea nao zaidi ya milioni moja wameyakimbia makazi yao.


Mwandishi:Thelma Mwadzaya AFPE/RTRE

Mhariri: Aboubakary Liongo