1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zaidi ya 50 wauawa nchini Iraq

Mohammed Khelef22 Desemba 2011

Huku viongozi wa kisiasa wa Iraq wakiwa katika mgogoro wa kimadaraka na kisheria, inaonekana vurugu zinazotokana na madhehebu zimeanza tena nchini humo, baada ya makumi ya watu kuuawa hivi leo katika miripuko ya mabomu.

https://p.dw.com/p/13XUo
Mashambulizi katika mji wa Kirkuk, Iraq.
Mashambulizi katika mji wa Kirkuk, Iraq.Picha: picture-alliance/dpa

Kwa mujibu wa wizara ya mambo ya ndani ya Iraq, jumla ya mashambulizi 11 yanayoonekana kupangwa vyema, yamewauawa kwa uchache watu 50 na kuwajeruhi wengine zaidi ya 170. Mashambulizi hayo yamefanywa asubuhi ya leo wakati watu wakikimbilia kazini katika kila kona ya mji mkuu, Baghdad.

Maafisa wa usalama wamesema maeneo yaliyoshambuliwa ni Allawi, Bab al-Muatham na Karrada yaliyo katikati ya Baghdad, Adhamiyah, Shuala na Shaab yaliyo upande wa kaskazini, Jadriyah upande wa mashariki, Ghazaliyah upande wa magharibi na Al-Amil na Dura kwa upande wa kusini.

Mauaji haya yamefanyika katika wakati wanasiasa nchini Iraq wakilumbana juu ya hati ya kukamatwa kwa makamo wa rais, Tariq al-Hashimi, ambapo Waziri Mkuu Nouri al-Maliki ameitaka mamlaka ya jimbo la Kurdi, kumkabidhi kiongozi huyo wa Kisunni kwa serikali yake, kukabiliana na mashitaka ya kupanga mashambulizi dhidi ya viongozi wa serikali.

Maliki aliuambia mkutano wa waandishi wa habari hapo jana, kuwa jimbo la Kurdi linalazimika kusaidia utawala wa sheria. "Tulimhukumu dikteta Saddam Hussein kwa kufuata utaratibu na haki, na tutahakikisha pia kuwa kesi ya Hashimi itafuata utaratibu na kuwa ya haki." Amesema Maliki.

Makamo wa Rais wa Iraq, Tariq Al-Hashimi
Makamo wa Rais wa Iraq, Tariq Al-HashimiPicha: picture-alliance/dpa

Lakini Hashimi, ambaye amekimbilia katika jimbo hilo lenye utawala wake wa ndani, amesema mashitaka hayo ni ya kisiasa, na akasema kuwa yuko tayari kushitakiwa kwenye jimbo la Kurdi, lakini sio na serikali ya Maliki, ambayo amesema imejaa rushwa. Hashimi ameikana rikodi ya sauti iliyorushwa na televisheni ya Iraq, ambayo ilikuwa inakiri kushiriki kwake kwenye mashambulizi, akiita kuwa ni ya kutunga.

Maliki, ambaye mwenyewe ni kutokea madhehebu ya Shia, ametaka pia Bunge limfute kazi naibu wake, Saleh al-Mutlak, baada ya kuiita serikali kuwa ni ya kidikteta. Kama alivyo Hashimi, Mutlak pia ni Sunni na anatoka chama cha Iraqiyya. Wakati huo huo, Iraqiyya wamegomea vikao vya bunge na vya baraza la mawaziri, na Maliki ametishia kuzijaza nafasi za mawaziri kwa kuteua wapya.

Kama itafanyika hivyo, hatua hiyo itamaanisha kuunda serikali ya upande mmoja na hivyo kuvunjika kwa serikali ya umoja wa kitaifa, iliyodumu kwa mwaka mmoja tu.

Waziri Mkuu wa Iraq, Nuri al-Maliki
Waziri Mkuu wa Iraq, Nuri al-MalikiPicha: picture-alliance/dpa

Marekani imezitaka pande zinazozozana kutumia busara na kuepusha vurugu. Mgogoro huu unakuja siku chache tu, baada ya majeshi ya Marekani kuondoka Iraq, na kuiacha nchi ambayo Rais Barack Obama aliita "iliyotulia, huru na inayojitegemea."

Licha ya Maliki na viongozi wengine kuitisha mazungumzo ya kutatua mgogoro huu, msemaji wa Waziri Mkuu huyo ameliambia shirika la habari la AFP kwamba, hatokubali muafaka wowote juu ya mashitaka yanayomkabili Hashimi.

Vurugu zimepungua sana kulinganisha na miaka ya nyuma nchini Iraq, lakini mashambulizi kama haya ya leo hufanyika mara kwa mara. Jumla ya watu 187 waliuawa katika vurugu za mwezi uliopita wa Novemba.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Saumu Yusuf