1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zaidi ya mahabusu 3,000 wachiliwa Pakistan

21 Novemba 2007
https://p.dw.com/p/CPlr

Pakistan hapo jana imesema imewaachilia huru zaidi ya mahabusu 3,000 waliotiwa mbaroni chini ya utawala wa hali ya hatari uliotangazwa na Rais Pervez Musharraf.

Katika hatua nyengine yenye lengo la kukomesha wiki kadhaa za machafuko ya kisiasa na hasira ya kimataifa tume ya uchaguzi ya Pakistan imetangaza kwamba uchaguzi mkuu wa bunge utafanyika nchini humo tarehe nane mwezi wa Januari.

Javed Cheema msemaji wa wizara ya mambo ya ndani ya Pakistan anasema tokea utawala wa hali ya hatari ulipotangazwa hapo tarehe 3 mwezi wa Novemba takriban mahabusu 3,416 wameachiliwa huru wakiwemo viongozi wa kisiasa na wafanyakazi wa kisiasa kadhalika mawakili na anataraji mahabusu takriban 2,000 wanaoendelea kushikiliwa wataachiliwa hivi karibuni katika mchakato huo unaoendelea.

Musharraf ambaye yuko ziarani Saudi Arabia ambapo hasimu wake mkuu Nawaz Sharif anaishi uhamishoni anakabiliwa na wito wa kimataifa kuondowa utawala wa hali ya hatari , kuwaachilia huru mahabusu,kuondowa vikwazo dhidi ya vyombo vya habari na kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na wa haki.