1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zaidi ya raia milioni 9 wa Syria hawana makaazi

Admin.WagnerD14 Machi 2014

Shirika la kushughulikia wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR limesema mzozo wa Syria umesababisha mzozo mkubwa zaidi duniani wa wakimbizi kwani umesababisha zaidi ya raia milioni 9 wa Syria kuachwa bila makaazi

https://p.dw.com/p/1BPeF
Picha: United Nation Relief and Works Agency/Reuters

Kamishna mkuu wa shirika hilo la UNHCR Antonio Guterres amesema asilimia 40 ya wasyria wameyatoroka makaazi yao huku zaidi ya milioni 6.5 kati yao wakitafuta hifadhi salama ndani ya Syria kwenyewe na wengine milioni 2.6 wakitorokea nchi jirani.

Guterres amesema ni jambo lisiloingia akilini ni vipi janga kubwa la kibinadamu la kiwango cha namna hiyo linajiri machoni mwa walimwengu bila ya hatua zozote za maana kuchukuliwa kuzuia umwagikaji mkubwa wa damu unaoendela Syria.

UNHCR imesema wengi wa wakimbizi wa Syria wamepata hifadhi katika nchi zisizo na utajiri mkubwa kama Misri,Iraq,Jordan,Lebanon,Uturuki na hivyo imeathiri pakubwa uchumi na miundo mbinu ya nchi hizo.

Chini ya asilimia nne ya wakimbizi wa Syria wako Ulaya

Ni kiasi kidogo cha wakimbizi wa Syria wameweza kutafuta hifadhi katika nchi za Ulaya kutokana na hatari ya kuzifika nchi hizo kupitia safari za majini na pia kukumbwa na hata hatari kubwa zaidi iwapo watanusirika ya kukataliwa na nchi hizo.

Kamishna mkuu wa UNHCR Antonio Guterres
Kamishna mkuu wa UNHCR Antonio GuterresPicha: Reuters

Guterres amesisitiza kutumika kwa kila juhudi kutafuta amani Syria ili kupunguza dhiki na mateso ya raia wasio na hatia waliojikuta katika mzozo huo na kulazimika kuyatoroka makaazi yao,jamii zao,kazi zao na maisha yao ya kawaida.

Vita hivyo vya Syria ambavyo vilianza mwezi Machi mwaka 2011 kama wimbi la uasi la kutaka kumg'oa madarakani Rais Bashar Al Assad limesababisha vifo vya zaidi ya watu 140,000 na kuziathiri pia nchi za kanda hiyo kutokana na mzigo wa kuwapokea wakimbizi.

Nchini Lebanon pekee idadi ya wakimbizi wa Syria inaelekea kufika milioni moja huku ikitarajiwa kuongezeka hadi milioni 1.6 ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.

UNHCR imezitaka nchi za Ulaya,Amerika ya Kaskazini na Asia kutoa nafasi kwa wakimbizi wa Syria.

Bunge la Syria laidhinisha sheria mpya za uchaguzi

Huku janga hilo la kibinadaamu likiendelea,bunge la Syria leo limeidhinisha sheria mpya za uchaguzi ambazo kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miongo mingi inaruhusu wagombea kadhaa kuwania urais.

Mpatanishi mkuu wa Syria Lakhdhar Brahimi
Mpatanishi mkuu wa Syria Lakhdhar BrahimiPicha: Reuters/Denis Balibouse

Sheria hiyo imeidhinishwa miezi michache kabla ya uchaguzi mkuu.Hata hivyo sheria hiyo inawazuia viongozi wa upinzani walio uhamishoni kugombea dhidi ya Assad kwani sheria hiyo inataka wagombea wawe wameishi Syria kwa miaka kumi mfululizo.

Rais Assad anatarajiwa kugombea muhula mwingine wa miaka saba.Uchaguzi sharti ufanywe kati siku sitni na tisini kabla ya muhula wake kukamilika tarehe 17 mwezi Julai mwaka huu.

Upande wa upinzani na wapatanishi wa kimataifa wamepinga kuandaliwa kwa uchaguzi mkuu huku bado mazungumzo ya kuvimaliza vita hivyo yakiwa bado yanaendelea.

Mpatanishi mkuu wa Umoja wa Mataifa na nchi za kiarabu kuhusu Syria Lakhdhar Brahimi akilihutubia baraza la usalama la Umoja wa Mataifa jana amesema anahofia kuwa iwapo kutakuwa na uchaguzi,upinzani hautakuwa na nia ya kufanya mazungumzo na serikali.

Mwandishi:Caro Robi/afp/dpa

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman