1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zaidi ya watu 10,000 wahofiwa kufariki Ufilipino

Mjahida11 Novemba 2013

Wanajeshi na polisi wa Ufilipino wamepelekwa katika miji ilioathirika na kimbunga kikali kuwahi kuipiga nchi hiyo ili kudhibiti wizi wa mali unaohatarisha juhudi za kutoa misaada ya kibinaadamu kwa waathirika.

https://p.dw.com/p/1AFCJ
Maafa ya Kimbunga Haiyan
Maafa ya Kimbunga HaiyanPicha: Reuters

Zaidi ya watu 10,000 wanahofiwa kufariki kutokana na kimbunga hicho kwa jina Haiyan kilichopiga kwa mawimbi mazito na upepo mkali na kusababisha athari kubwa nchini Ufilipino siku ya Ijumaa, huku mji wa Tacloban ukiwa moja ya miji ilioathirika pakubwa.

Waokoaji kwa sasa wanajaribu kupeleka misaada ya chakula na malazi kwa waathirika wa kimbunga hicho katika mji huo ulio na idadi ya watu 220,000.

Hata hivyo hatua hiyo iliendeshwa kwa changamoto kubwa kutokana na wizi uliokuwa ukiendelea. Waporaji walivunja maduka pamoja na kuvamia gari la misaada la msalaba mwekundu na kuchukua vile vilivyokuwemo ndani.

Baadhi ya waathiriwa ambao ni wafanyabiashara wadogo pia wameripoti kuibiwa kwa televisheni, na mashini za kufulia nguo. Kulingana na msemaji wa wizara ya ulinzi wa raia nchini humo, Reynaldo Balido, kurejesha usalama na hai ya utulivu katika mji huo wa Tacloban, ni moja ya mambo wanayoyapa kipaumbele.

Wakaazi wakichukua mali kutoka kwa baadhi ya maduka
Wakaazi wakichukua mali kutoka kwa baadhi ya madukaPicha: Reuters

Akizungumza na shirika la habari la AFP hapo jana, Andrew Pomeda, aliye na umri wa miaka 36, na mwalimu wa shule moja ya upili mjini humo, amesema watu kwa sasa wamegeuka kuwa wahalifu, kwa kuingia katika majengo ya kibiashara kuiba chakula na mali. Pomeda amesema ana hofu kwamba kwa muda wa wiki moja watu watakuwa wanauana kutokana na njaa.

Jeshi la Marekani lajiunga katika shughuloi za uokozi

Wakati huo huo, jeshi la Marekani limeungana na wenzao wa Ufilipino kuendeleza juhudi ya kuwatafuta manusura wa Kimbunga Haiyan. Siku nne baada ya kimbunga hicho kuikumba nchi hiyo na kusababisha maelfu ya miili kutapakaa kote barabarani, sasa waathirika wana mahitaji makubwa ya chakula, maji, matibabu na malazi.

Joan Lumbre-Wilson mkaazi wa mji wa Tacloban amesema kinachohitajika kwa sasa ni kundi lililojipanga ambalo litajishughulisha na zoezi la kuondoa miili iliyotapakaa barabarani na pia kusimamisha wizi mkubwa wa mali ya watu unaoendelea.

Waokozi wakiwasaidia waathirika
Waokozi wakiwasaidia waathirikaPicha: picture-alliance/dpa

Eneo jengine lililoathirika ni mji wa Samar ambapo Gavana wa mji huo amethibitisha kuuwawa kwa watu 433 na kusema idadi hiyo huenda ikaongezeka.

Huku hayo yakiarifiwa, watu 10 wanasemekana kufariki, 67 wamejeruhiwa huku wengine 39,000 wakihamishiwa katika maeneo salama baada ya kimbunga hicho Haiyan kusababisha mvua kubwa nchini Vietnam, hasa katika maeneo ya kaskazini mashariki na katikati mwa nchi hiyo.

Mwandishi:Amina Abuakar/AFP/dpa

Mhariri: Mohammed Khelef