1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zaidi ya watu 30 wauwawa na wengine 100 kujeruhiwa katika milipuko ya bomu Damascus

23 Desemba 2011

Milipuko miwili imesikika mjini Damascus leo kabla ya kuanza kwa maandamano ya kuupinga ujumbe wa wangalizi wa jumuiya ya Kiarabu uliowasili nchini humo hapo jana kwa lengo la kumaliza umwagikaji damu

https://p.dw.com/p/13Y9M
Waandamanaji katika mji wa Homs Syria
Waandamanaji katika mji wa Homs SyriaPicha: AP

Mabomu hayo yamelenga kambi mbili za kiusalama katika mji huo mkuu ambapo televisheni ya taifa inalinyooshea kidole cha lawama kundi la kigaidi la Al qaeda. Walioshuhudia wamesema gari la walipuaji wa kujitoa muhanga lilijaribu kuingia kwa nguvu ndani ya jengo la usalama wa kitaifa, huku nalo gari jingine likilipuka mbele ya jengo la huduma za usalama katika eneo hilo.

Hayo yanajiri huku ghasia zikiripotiwa kuendelea katika mikoa ya kati na kaskazini magharibi mwa Syria ambapo watu sita wameripotiwa kuuwawa usiku wa kuamkia leo. Wanaharakati nchini humo wameitisha maandamano makubwa hii leo baada ya sala ya Ijumaa ya kuupinga ujumbe wa waangalizi wa jumuiya ya Kiarabu ambao uliwasili nchini humo hapo jana kwa lengo la kumaliza umwagikaji damu.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Syria, Walid Muallem, amesema wanatumai waangalizi hao wataondoa ubishi wa serikali yake kuwa machafuko hayo ni kazi ya magenge ya kigaidi, na wala siyo kwamba wanawazidi nguvu waandamanaji wa amani jinsi inavyosisitizwa na mataifa ya magharibi na mashirika ya kutetea haki za binadamu.

Ujumbe huo wa waangalizi unatarajiwa kusimamia mpango wa Jumuiya ya Kiarabu wa kumaliza miezi tisa ya umwagikaji damu ambapo  zaidi ya watu 5,000 wameuwawa kulingana na umoja wa mataifa, ikiwa ni zaidi ya maafisa 2,000 wa usalama kwa mujibu wa ripoti za serikali.

Wanachama wa jumuiya ya Kiarabu
Wanachama wa jumuiya ya KiarabuPicha: dapd

Lakini ujumbe huo umezua pingamizi kali kutoka kwa wanaharakati wanaodai kuwa hiyo ni mbinu ya kukwamisha hatua thabiti dhidi ya ukandamazaji wa umwagikaji damu wa serikali na wakaitisha maandamano ya kitaifa.

Mwanaharakati mmoja amesema hakuna kile kinachoweza kusitisha mauaji yanayofanywa na utawala wa rais Bashar Al Assad hadi pale mzozo huo ukabidhiwe baraza la usalama la umoja wa mataifa. Viongozi wa upinzani wameutaja mwafaka wa Syria katika ujumbe huo kuwa njama mpya ya kuizuia jumuiya ya Kiarabu dhidi ya kuupeleka mzozo huo kwa baraza la usalama la umoja wa mataifa.

Licha ya kuwasili kwa kundi hilo la mwanzo, wanaharakati wamesema mapambano kati ya wanajeshi walioitoroka serikali na wanajeshi watiifu katika maeneo ya kivita ya Homs na Idlib yaliendelea usiku kucha, na kuwauwa takriban watu sita.

Mwanaharakati mmoja Ahmed Abdallah amesema watu watano kutoka familia moja waliuwawa katika mji wa Idlib. Shirika la kutetea haki za binadam la Syria Observatory for Human Rights lilitoa mkanda wa video ukionyesha maiti 49 ya wanaume inalodai waliuwawa Idlib na vikosi vya serikali siku ya jumanne.

Ghasia hizo ziliifanya wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani mjini Berlin kumtaka balozi wa Syria nchini humo kusitisha mara moja ukandamizaji huo wa kinyama dhidi ya waandamanaji wanaotaka demokrasia.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA

Mhariri: Josephat Charo