1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zaidi ya watu 40 wauawa Afghanistan.

Halima Nyanza26 Agosti 2009

Muda mfupi tu, baada ya Afghanistan kuanza kutoa matokeo ya uchaguzi mkuu wa Rais, imeripotiwa kwamba watu 43 wameuawa kufuatia shambulio la bomu lililotokea katika mji wa kusini mwa nchi hiyo wa Kandahar.

https://p.dw.com/p/JIWl
Licha ya kuimarishwa kwa ulinzi katika kipindi hiki cha uchaguzi nchini Afghanistan, mashambulio ya mabomu bado yanaendelea na kuuawa watu wasio na hatia.Picha: DW/Arkadi Dubnow

Zaidi ya watu 65 wamejeruhiwa baada ya bomu lililotegwa katika lori kulipuka katikati ya mji huo wa Kandahar, wakati watu wakifuturu, katika kipindi hiki cha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Kamanda wa polisi katika kanda ya kusini mwa nchi hiyo Jenerali Ghulam Ali Wahdat amesema eneo hiklo bado limezuiwa ili kuwezesha majeshi ya ulinzi kufanya uchunguzi.

Shambulio hilo la bomu ambalo maafisa wa nchi hiyowanadai kufanywa na wapiganaji wenye uhusiano na Taliban lililipuka karibu na kampuni ya Ujenzi ya Japan na ofisi nyingine za serikali na kusababisha madhara kadhaa ikiwemo watu kunasa kwenye vifusi.

Hata hivyo msemaji wa Taliban Qari Yousef Ahmadi amekanusha kuhusika na shambulio hilo na kusema kuwa kundi hilo la wapiganaji limelaani mauaji hayo ya raia wasio na hatia.

Shambulio hilo limetokea muda mfupi tu, baada ya Tume ya uchaguzi ya nchi hiyo kutangaza matokeo ya kwanza ya uchaguzi wa Rais uliofanyika Alhamisi iliyopita, chini ya vitisho vilivyotolewa na Taliban, ambapo leo tena afisa mmoja wa katika jimbo la Kunduz amekufa baada ya kulipukiwa na bomu wakati akienda kazini.

Matokeo ya awali yaliyokwisha tolewa yanaonesha kwamba Rais Hamid Karzai, ambaye ametokea katika jimbo la Kandahar, anaongoza kwa asilimia mbili juu ya mpinzani wake mkubwa Waziri wa zamani wa Mambo ya Nchi za Nje wa nchi hiyo Abdullah Abdullah.

Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo imesema Rais Karzai anaongoza kwa kupata asilimia 41 ya kura zote zilizopigwa ukilinganisha na takriban asilimia 39 alizopata Abdullah.

Mchuano wa karibu kati ya wagombea hao wawili wa Urais nchini humo, umekuwa ukiongeza upinzani mkali, huku kukiwa na madai ya kufanyika kwa udanganyifu, katika hali ya kumpendelea Rais Karzai, ambaye kambi yake imedai kushinda uchaguzi huo, muda mfupi tu baada ya kumalizika kwa zoezi hilo la kupiga kura.

Mpaka sasa ni asilimia 10 tu ya kura ndio zilizokwisha hesabiwa.

Katika uchaguzi huo watu wachache walijitokeza kupiga kura kutokana na wasiwasi wa hali ya usalama, ikiwa ni moja ya malengo ya Taliban ya kampeni zake za kuwatisha wananchi ili wasiweze kujitokeza kwa wingi kwenda kupiga kura, hali itakayodhoofisha matokeo ya uchaguzi huo.

Mwandishi: Halima Nyanza(AFP, AP)

Mhariri:Abdul-Rahman