1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zain kuuzwa kwa Bharti Airtel

Kabogo Grace Patricia16 Februari 2010

Itakapouzwa kampuni hiyo itapata faida ya hadi dola bilioni 5

https://p.dw.com/p/M3E9
Simu ya mkononi ambayo imekuwa na matumizi makubwa sana duniani kote.Picha: DW / Bergmann

Kampuni ya simu ya Kuwait ya Zain imesema inatarajia kupata faida ya hadi dola bilioni tano kutokana na kuuza mitambo ya kampuni hiyo barani Afrika kwa kampuni ya India ya Bharti Airtel kwa dola bilioni 10.7.

Kulingana na makubaliano yaliyofikiwa, kampuni ya Bharti Airtel inatakiwa kulipa dola milioni 10 wakati mpango huo utakapokamilika na dola milioni 700 zilizobakia zitalipwa mwaka mmoja baada ya mkataba kusainiwa. Taarifa iliyotolewa na kampuni hiyo ya Kuwait katika mtandao wa Soko la Hisa la Kuwait, imeeleza kuwa uuzaji wa huduma zake katika mataifa 15 ya Afrika utaongeza hisa za kampuni hiyo zisizo na riba ya kudumu kwa dola bilioni tisa. Hata hivyo mchakato wa kuuza mitambo hiyo hautazihusisha nchi za Sudan na Morocco.

Bodi ya wakurugenzi ya Zain itafanya majadiliano yake maalum na kampuni ya Bharti Airtel hadi Machi 25, mwaka huu kwa ajili ya kuukamilisha mkataba huo. Makubaliano ya kuuzwa kwa kampuni ya Zain yalipitishwa kwa pamoja na bodi ya wakurugenzi wa kampuni hiyo katika mkutano uliohudhuriwa na mwakilishi wa serikali ambayo ina hisa ya asilimia 24.6, ikiashiria uungwaji mkono wa serikali ya Kuwait katika uuzaji wa kampuni hiyo.

Kampuni ya Zain ilijiingiza katika soko la Afrika mwaka 2005, ikiwa imenunua kampuni ya simu ya Celtel kutoka kwa kampuni ya Kiholanzi kwa dola bilioni 3.5. Baadaye Zain ikapata tamaa ya kuongeza soko lake kubwa katika nchi nyingine za Afrika ikiwemo Nigeria na kuongeza pia huduma zake Mashariki ya Kati ambapo iliwekeza kiasi dola bilioni 12. Zaidi ya nusu ya faida ya Zain kwa mwaka uliopita ilitokana na wateja wa barani Afrika.Kikanda, Zain inaendesha huduma zake huko Bahrain, Iraq, Jordan, Lebanon na Saudi Arabia pamoja na Kuwait.

Endapo mkataba huo utafikiwa, utafanikiwa kumaliza miaka mingi ya mafanikio ya kupanua huduma za kampuni hiyo iliyokuwa ikiongozwa na mkurugenzi wake Saad al-Barrak, aliyejiuzulu mwanzoni mwa mwezi huu na nafasi yake kuchukuliwa na Nabil bin Salamah. Barrak aliyeteuliwa kuiongoza kampuni hiyo mwaka 2002 alikuwa na matarajio ya kuifanya kampuni hiyo kuwa miongoni mwa kampuni bora 10 za simu zinazoongoza duniani kote ifikapo mwaka 2012. Lakini mipango yake hiyo ilikwaa kisiki nchini Saudi Arabia na katika mataifa mengi ya Afrika ambako inaendesha huduma zake. Miongoni mwa nchi ambazo kampuni hiyo ya simu za mkononi ya Zain imekuwa na mafanikio ni Tanzania, ambako kuna makampuni mengi ya simu za mkononi.

Kwa sasa kampuni ya simu ya Zain ni ya tatu katika eneo la Ghuba ikiwa nyuma ya kampuni ya simu ya Saudi Arabia ya Saudi Telecom na kampuni ya simu ya Etisalat ya Umoja wa Falme za Kiarabu.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFP)

Mhariri:M. Abdul-Rahman