1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ZANU PF yamshinikiza Mugabe ajiuzulu

Caro Robi
18 Novemba 2017

Chama tawala Zimbabwe ZANU PF kimemtaka Rais Robert Mugabe ajiuzulu. Gazeti la Herald limeandika kuwa matawi ya chama hicho katika majimbo yote10 yalikutana Ijumma na yamemtaka Mugabe na mke wake Grace wajiuzulu.

https://p.dw.com/p/2nqli
Simbabwe Harare Robert Mugabe
Picha: picture-alliance/AP Photo/B. Curtis

Viongozi wa chama hicho wamesema watamshinikiza kiongozi huyo ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 1980 kuondolewa kutoka uongozi wa chama hicho ifikapo hapo kesho Jumapili, na baada ya hilo, bunge litapiga kura ya kutokuwa na imani naye.

Chama cha ZANU PF kitafanya mkutano maalamu wa kamati kuu siku ya Jumapili kujadili yanayojiri kisiasa nchini humo.

Mugabe alionekana kwa mara ya kwanza hadharani, katika mahafali ya chuo kikuu mjini Harare siku ya Ijumaa (17.11.2017) tangu jeshi lilipomuweka chini ya kifungo cha nyumbani wiki hii. Mkewe Grace hajaonekana hadharani tangu jeshi lilipochukua madaraka.

Jeshi la Zimbabwe linapata ugumu wa kuonyesha heshima kwa kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 93 kwa kumuita rais na kamanda mkuu wa jeshi.

Madaraka mikononi mwa Jeshi

Taarifa kutoka kwa jeshi hilo imesema kuwa viongozi wake wanashauriana na Kamanda Mkuu wa jeshi Rais Robert Mugabe kuhusu njia bora ya kusonga mbele na litalifahamisha taifa baadaye kuhusu matokeo hayo haraka iwezekanavyo.

Kituo cha televisheni cha serikali ZBC kimeripoti kuhusu kuendelea kwa shinikizo kutoka kwa wanachama wa ZANU PF kwa Mugabe kujiuzulu. ZBC imekuwa ikitumika na serikali ya Mugabe kwa miongo kadhaa kueneza propaganda.

ZANU PF pia imeitisha maandamano Jumamosi (18.11.2017) katika mji mkuu, Harare kuliunga mkono jeshi kwa kuchukua madaraka na kumshinikiza Mugabe ajiuzulu. Gazeti la Herald limeripoti kuwa chama hicho kinataka makamu wa Rais aliyefutwa kazi Emmerson Mnangagwa arejeshwe katika wadhifa huo kwasababu alifutwa kazi bila ya ridhaa ya kamati kuu ya chama hicho.

Wazimbawe wengi wanahisi mipango ya jeshi ni kumkabidhi Mnangagwa madaraka. Huenda viongozi wa kijeshi wanasubiri Mnangagwa ambaye anajulikana kwa jina maarufu kama mamba arejeshwe katika wadhifa wa makamu wa rais kabla ya kumshinikiza Mugabe kuondoka madarakani kwa njia ya amani.

Mugabe anaheshimika sana kama kiongozi aliyepigania uhuru lakini pia wengi wanamuona kama Rais aliyeivuruga nchi yake kwa kusalia madarakani kwa muda mrefu.

Mugabe ameiongoza Zimbabwe tangu 1980

Uchumi wa nchi hiyo umeporomoka vibaya, visa vya ufisadi, usimamizi mbaya, azma ya mke wake Grace kutaka kurithi madaraka na umri wake kuwa mkubwa ni mambo yanayowafanya Wazimbabwe kuhisi hana uwezo tena wa kuliongoza taifa hilo.

Zimbabwe Mugabe Rally
Mugabe na mke wake GracePicha: picture-alliance/AP Photo/T.Mukwazhi

Rais wa Botswana Ian Khama amemtaka ajiuzulu akisema hadhani kama kuna mtu yeyote anayestahili kuwa madarakani kwa muda mrefu kama Mugabe akiongeza wao ni marais na sio wafalme.

Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma ambaye aliongoza kikao cha viongozi wa jumuiya ya ushirikiano wa maendeleo wa nchi za Kusini mwa Afrika SADC mjini Gaberone, Botswana amesema wanafuatilia kwa wasi wasi mkubwa matukio ya kisiasa yanayojiri Zimbabwe na anatumai hayatasababisha kuingia madarakani kwa utawala usiotambulika kikatiba.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Rex Tillerson aliwaambia mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za Afrika wanaohudhuria mkutano mjini Washington kuwa anahimiza kurejea haraka kwa utawala wa kiraia Zimbabwe akisema nchi hiyo ina fursa ya kuanzisha njia mpya ambayo sharti ihusishe chaguzi zinazoendeshwa kwa njia ya kidemokrasia na kuheshimu haki za binadamu. China imesema inatumai kuwa hali ya kisiasa inayoendelea Zimbabwe itasuluhishwa kuambatana na sheria na uthabiti uterejea nchini humo.

Mwandishi: Caro Robi/Reuters/ap

Mhariri: Grace Kabogo