1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zelensky ziarani Slovakia kabla ya kuelekea Uturuki

Angela Mdungu
7 Julai 2023

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amekutana na kufanya mazungumzo na Rais Zuzana Caputova wa Slovakia leo mchana. Ziara hiyo ni mfululizo wa safari za Zelensky za kutaka kuungwa mkono ili kujiunga na Jumiya ya NATO.

https://p.dw.com/p/4TbAf
Ukraine Präsident Wolodymyr Selenskyj
Picha: Ukrainian Presidency via/abaca/picture alliance

Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine aliwasili katika mji mkuu wa Slovakia, Bratislava  kabla ya kuelekea Uturuki ambako pia anatazamiwa kufanya mazungumzo na Rais Recep Tayyip Erdoga leo. Ziara yake Slovakia aliitangaza mwenyewe kupitia katika ukurasa wake wa mtandao wa Twitter.

Mada kuu kwenye mkutano wake alioufanya na rais  Zuzana Caputova ni kutafuta kungwa mkono zaidi kijeshi na dhamira ya kujiunga na Umoja wa Ulaya pamoja na Jumuiya ya kujihami ya NATO. Rais Caputova ni kati ya viongozi wa Ulaya walio mstari wa mbele katika kuiunga mkono Ukraine.

Rais huyo ameshawahi kuitembelea Kyiv mara mbili tangu ilipoingia kwenye mzozo na Urusi na amewahi kuyatembelea maeneo ambayo yameathiriwa zaidi na mgogoro huo akiwa sambamba na Zelensky. 

Rais wa Slovakia Zuzana Caputova
Rais wa Slovakia Zuzana CaputovaPicha: Radovan Stoklasa/REUTERS

Katika ziara mkutano wao wa leo, Zelensky pia ameitolea wito jumuiya ya kujihami ya NATO ishughulikie masuala ya azma ya Sweden na Ukraine kujiunga na jumuiya hiyo na kuongeza kuwa, kutokuwa na uamuzi kuhusu suala hilo kunatishia uimara wa jumuiya hiyo na usalama wa dunia.

Wanachama wa NATO kuungana kuisaidia Ukraine kujiunga na jumuiya hiyo

Katika hatua nyingine, katibu mkuu huyo wa jumuiya ya kujihami ya NATO Jens Stoltenberg amesema kuwa mkutano wa wiki ijayo wa jumuiya hiyo utatafuta njia ya kuisaidia Ukraine kuwa mwanachama.

Katibu mkuu wa NATO  Jens Stoltenberg
Katibu mkuu wa NATO Jens StoltenbergPicha: François Walschaerts/AFP

Stoltenberg amezungumzia pia suala la kupeleka silaha tata, zinazopingwa na makundi ya haki za binadamu za mabomu ya mtawanyiko. Amesema, ni juu ya washirika binafsi kuamua ni aina gani ya wanapaswa kupeleka Ukraine.

Wakati huo huo, vyombo vya habari vya Urusi vimeripoti kwamba, serikali ya nchi hiyo inafikiria kufanyika kwa mkutano kati ya rais Vladimir Putin na mwenzake wa Urusi, Recep Tayyip Erdogan, ingawa bado tarehe maalumu kwa ajili ya tukio hilo haijapangwa.