1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ziara kuponesha vidonda vya zamani

P.Martin8 Oktoba 2007

Azma ya ziara ya vizazi vya kamanda wa enzi ya ukoloni ya Ujerumani nchini Namibia,Lothar von Trotha,alie na sifa mbaya,ni kusaidia kuponesha madonda ya zamani.

https://p.dw.com/p/C7iP

Ziara ya upatanisho ya familia ya von Trotha haikupokewa mikono wazi na vizazi vyote vya Herero.Ziara hii ni tukio la mkutano uliofanywa nchini Ujerumani kati ya familia ya von Trotha na Chifu wa kabila la Herero,Alfons Maharero ambae ni kizazi cha Samuel Maharero alieongoza jeshi la Waherero vitani.

Juma lililopita,familia ya von Trotha ilipokwenda Namibia,iliuambia ujumbe wa Waherero uliowapokea kuwa wanaona aibu kwa maovu yaliyotokea miaka 100 iliyopita.Wolf-Thilo von Trotha alisema: „Tunasikitika mno kwa yale yaliyowafikia watu wenu na hata makabila ya Nama na Damara-vifo katili vya maelfu ya wanaume,wanawake na watoto ambavyo haviwezi kutetewa.“ Mwisho wa nukulu.

Katika mwaka 1904,vikosi vya Von Trotha vilifuata amri ya kuangamiza ili kuzima uasi wa kabila la Herero na vilisababisha vifo vya maelfu ya watu wa Herero.

Ingawa Halmashauri ya Ovaherero iliyoundwa kuhusu mauaji hayo ya halaiki,imeisifu ziara hiyo kama ni nafasi ya kuponesha vidonda vya zamani na ni ya upatanisho,Chifu Mkuu wa Herero,Kuaima Riruako alitangaza bungeni kuwa hatokaa meza moja na kizazi cha von Trotha.Amesema,ikiwa familia hiyo inataka kusafisha jina lake,basi waieleze serikali ya Ujerumani makosa yaliyofanywa na wazazi wao.

Riruako anajaribu kuishinikiza serikali ya Ujerumani kufidia maovu yaliyofanywa dhidi ya watu wake katika enzi ya ukoloni.Hadi hivi sasa, hakufanikiwa na juhudi za kuishtaki serikali ya Ujerumani katika mahakama ya Marekani.

Serikali ya Ujerumani,mara kwa mara imeeleza kuwa inajitahidi kutekeleza wajibu wake wa kihistoria kwa kuwa mfadhili mkubwa kabisa wa Namibia na itaisaidia Namibia kama taifa moja na si kundi moja la kikabila.Majeshi ya kikoloni ya Ujerumani vile vile yalipigana vita vikali dhidi ya makabila mengine ya Namibia kama Nama na Damara.

Cheo cha chifu mkuu wa Herero hakikuwepo enzi ya ukoloni wa Ujerumani,kati ya mwaka 1884 na 1919.Von Trotha alikuwa kamanda wa majeshi ya kifalme ya Ujerumani mnamo mwezi Mei mwaka 1904.Baadae Namibia ikawa chini ya uongozi wa serikali ya ubaguzi ya Afrika Kusini na imepata uhuru wake mwaka 1990.