1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ziara ya Blair Mashariki ya kati kama mjumbe maalum katika kutafuta suluhu mashariki ya kati

23 Julai 2007

Waziri mkuu wa zamani wa Uingereza Tony Blair yuko nchini Israel ikiwa ni ziara yake ya kwanza katika eneo hilo tangu kuteuliwa kuwa mjumbe maalum wa Mashariki ya kati.

https://p.dw.com/p/CB2Z
Tony Blair
Tony BlairPicha: AP

Blair ambaye pia ametembelea Jordan anatarajia kutia shime zaidi juhudi za kuleta amani kati ya wapalestina na waisrael.

Tony Balir ambaye sasa ni mjumbe maalum katika mazungumzo ya kutafuta amani mashariki ya kati aliwasili Israel hii leo mchana ikiwa ni mara yake ya kwanza kufika nchini humo tangu kuteuliwa katika wadhifa huo mpya.

Atakutana leo hii na waziri wa mambo ya nje wa Israel Tzipi Livni na waziri wa ulinzi Ehud Barak na hapo kesho amepangiwa kukutana na waziri mkuu Ehud Olmert pamoja na rais Mahmoud Abbas nawaziri mkuu wa Palestina Salam Fayad.

Blair ametokea Jordan ambako alikaa kwa muda mfupi na kukutana na waziri wa mambo ya nje Abdullah al Khatib.

Kwa mujibu wa maafisa nchini Jordan bwana Blair alisikiliza maoni ya Jordan juu ya kuanzisha tena mpango wa amani ya mashariki ya kati.

Maafisa wa pande zote mbili zinazozozana Palestina na Israel wamekiri kwamba Tony Blair anakabiliwa na vizingiti na makubaliano ya amani yanaweza tu kufikiwa kwa njia ya mazungumzo ya moja kwa moja.

Mpatanishi wa Palestina katika mzozo huu Saeb Erekat amesema maamuzi yanayohitajika katika suala la amani hayawezi kutoka kwa wajumbe ila kwa wenyewe wapalestina na waisraeli.

Msemaji wa Tony Blair Matthew Doyle amearifu kuwa mkutano kati ya Blair na waziri wa nje wa Jordan ulikuwa wa mafanikio ambapo Jordan ilikaribisha uteuzi wa Blair kama mjumbe maalum na kuahidi kushirikiana naye katika juhudi hizo za kutafuta suluhu ya mzozo wa mashariki ya kati.

Hata hivyo Mathew amekataa kuzungumzia kwa undani juu ya mkutano huo baina ya Blair na Khatib lakini amesema Tony Blair hawezi kukutana na Kundi la Hamas ambalo linadhibiti ukanda wa Gaza baada ya mapambano makali na Fatah.

Kwa upande wake waziri wa mambo ya nje wa Jordan Abdillah Khatib amesema ziara ya Blair ina umuhimu kwa wapalestina,waisrael na eneo zima kwa jumla na kusisitiza wito wa Jordan wa kutaka paweko haki kwa wapalestina.

Amesema ili amani iweko kwenye eneo hilo inahitajika nguvu kwa wapalestina kujenga taasisi zao za serikali zitakazowawakilisha wapalestina wote na kuimarisha uchumi pamoja na sheria.

Uteuzi wa bwana Blair kama mjumbe maalum katika mashariki ya kati mwishoni mwa mwezi juni ulifurahiwa na Israel na baadhi ya wapalestina wanaoegemea upande wa rais Mahmoud Abbas wanaonekana kuwa na siasa za wastani lakini ulipingwa vikali na kundi la Hamas lilona usemi mkubwa Palestina kundi hilo likisema Blair ni rafiki wa karibu wa Israel na Marekani.

Blair anatajwa kuwa mtu anayeweza kuleta mabadiliko katika mzozo wa mashariki ya kati hasa ikizingatiwa alifaulu kuleta maridhiano huko Ireland kaskazini baina ya makundi hasimu ya wakristo wa madhehebu ya wakatoliki na waprotestanti ambapo hatimaye yalimaliza mzozo na kugawana madaraka serikalini.