1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ziara ya Bush Latin Amerika yakumbana na maandamano kadha.

9 Machi 2007

Mwanzoni mwa ziara ya rais Bush ya mataifa matano ya Amerika ya kusini imezusha maandamano katika eneo hilo, huku maelfu ya waandamanaji na polisi wakipambana nchini Brazil na wanafunzi nchini Colombia wakirusha milipuko dhidi ya maafisa.

https://p.dw.com/p/CHIZ

Zaidi ya wanafunzi 6,000, wanamazingira na Wabrazil wengi wenye kuelemea mrengo wa shoto walifanya maandamano ambayo kwa kiasi kikubwa yalikuwa ya amani katikati ya jiji la Sao Paulo kabla ya polisi kuwafyatulia mabomu ya kutoa machozi na kuwapiga na virungu.

Mamia walikimbia na kujificha katika maeneo mbali mbali ya kibiashara ili kuepuka ghasia, baadhi wakiwa wanatoka damu. Maafisa hawakutoa idadi ya majeruhi , lakini vyombo vya habari vya Brazil vimesema kiasi watu 18 wamejeruhiwa na picha zinaonyesha watu waliojeruhiwa wakiwa wanapelekwa katika magari ya hospitali.

Waandamanaji wanasema kuwa mvutano ulianza baada ya waandamanaji wenye msimamo mkali walipowachokoza polisi kwa kuwarushia mawe na vimbo, lakini wamesema pia kuwa polisi walijibu hali hiyo kwa nguvu kupita kiasi.

Wakati huo huo ripoti iliyotolewa na taasisi ya majadiliano kwa mataifa ya Amerika yenye makao yake makuu mjini Washington , inadai kuwa sera za Marekani katika kupambana na rais wa Venezuela Hugo Chavez imeonyesha mbinu dhaifu ama kutokuwa na mwendelezo wakati Chavez anaendelea kupambana na agenda za Marekani katika Latin Amerika.

Ripoti hiyo iliyopewa jina la Hugo Chavez , mtihani kwa ajili ya sera za Marekani, inapendekeza mtazamo wa mwambatano zaidi kuhusiana na uhusiano wa Marekani na Venezuela pamoja na juku mu lake katika Amerika ya kusini.

Pamoja na Brazil, Uruguay na Colombia, Bush atazuru pia Guatemala na Mexico katika ziara yake hiyo, ambayo inamalizika siku ya Jumatano wiki ijayo. Ikulu ya Marekani inakana kuwa ziara ya Bush si ziara ya kumpinga Chavez, lakini Bush amesisitiza kuwa Marekani inaleta ujumbe wa kufungua masoko na uwazi kwa serikali za eneo hilo.

Nchini Colombia ambako Bush anatarajiwa kuwasili siku ya Jumapili kwa ziara ya saa 7, wanafunzi , vyama vya upinzani na vyama vya wafanyakazi wamekuwa wakifanya maandamano kwa muda wa siku mbili kupinga ziara ya rais Bush.

Maafisa wamesema kuwa wanafunzi katika chuo kikuu cha Bogota walirusha mawe na milipuko kwa polisi, ambao walijibu kwa kuwafyatulia maji wakiwazuwia kufanya uharibifu na kuharibu utaratibu wa usafiri mjini humo.

Ziara ya rais Bush ya Marekani ya kusini na tangazo la mwanzoni mwa wiki hii la kutoa misaada zaidi bara hilo imeonekana kama juhudi za kuimarisha serikali zinazochukua msimamo wa kati na kupunguza ushawishi wa tawala za mrengo wa shoto ambazo zimeongeza upinzani wao dhidi ya Marekani, ikiwa ni pamoja na ule wa rais wa Venezuela Hugo Chavez.

Jana Alhamis mjini Buenos Aires Chavez amesema kuwa Bush anapaswa kupewa medali ya dhahabu kwa unafiki katika ziara yake hii ya kusini mwa bara la Amerika. Chavez ataongoza mkutano katika mji mkuu wa argentina utakaoingiliana na kuwasili kwa Bush katika nchi jirani ya Uruguay hii leo.