1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ziara ya Clinton Pakistan yagubikwa na mripuko

28 Oktoba 2009

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton leo ameanza ziara yake ya siku tatu nchini Pakistan.

https://p.dw.com/p/KHUJ
Secretary of State-designate Sen. Hillary Rodham Clinton, D-N.Y., listens to President-elect Barack Obama as he announces his national security team at a news conference in Chicago, Monday, Dec. 1, 2008. (AP Photo/Charles Dharapak)
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton.Picha: AP

Ziara hiyo ya Hillary Clinton inafanywa huku Pakistan ikizidi kukabiliwa na mashambulizi ya kigaidi. Clinton ni afisa wa ngazi ya juu kabisa wa Marekani kuitembelea Pakistan,tangu Rais wa Marekani Barack Obama kuvipa kipaumbele vita dhidi ya Taliban na Al Qaeda nchini Pakistan na Afghanistan. Alipowasili, Clinton alisifu operesheni za majeshi ya Pakistan dhidi ya wanamgambo wa Taliban na Al-Qaeda katika wilaya ya Waziristan ya Kusini.

Lakini ziara hiyo imegubikwa na mripuko mkubwa uliotokea katika soko lililojaa watu mjini Peshawar, muda mfupi tu baada ya Clinton kuwasili Pakistan. Shambulizi hilo katika mji huo mkuu wa wilaya ya Kaskazini-Magharibi umeua zaidi ya watu 80 na wengi wamenasa chini ya vifusi vya majengo yaliyoporomoka na kushika moto. Vile vile zaidi ya watu 150 wamejeruhiwa.

Mashambulizi ya wanamgambo wa Taliban yanayolenga raia na vituo vya kijeshi yameshika kasi tangu kuanzishwa kwa operesheni ya majeshi ya Pakistaninayolenga kuwatimua wanamgambo wa Taliban na Al-Qaeda kutoka Waziristan ya Kusini, eneo linalopakana na Afghanistan. Eneo hilo ni kitovu cha ugaidi nchini Pakistan. Marekani inayopambana na Wataliban katika nchi ya jirani Afghanistan, inaitegemea Pakistan kuwapiga vita wanamgambo hao na kuleta utulivu katika kanda hiyo. Wakati huo huo Pakistan nayo inaitegemea Marekani kwa msaada wa fedha na silaha ili kuweza kupambana na ugaidi unaozidi kushika kasi katika kila pembe ya nchi.

Lakini makombora ya Marekani yanayolenga vituo vya wanamgambo wa Al-Qaeda na Taliban katika ardhi ya Pakistan yamesababisha chuki miongoni mwa Wapakistani na serikali kutuhumiwa kuwa ni kibaraka cha Marekani. Wadadisi wanasema,serikali ya kiraia ya Pakistan iliyo madarakani zaidi ya mwaka mmoja baada ya utawala wa kijeshi wa miaka tisa, sasa inahitaji kuonyesha kuwa ushirikiano wake na Marekani ni wa manufaa.

Wakati wa ziara hii ya Clinton, inatazamiwa kuwa kutatiwa saini makubaliano ya uwekezaji, hasa katika sekta ya nishati. Clinton ameshakutana na waziri mwenzake wa Pakistan na hivi punde walikuwa na mkutano pamoja na waandishi wa habari.

Mwandishi:P.Martin/DPAE/AFPE

Mhariri: M.Abdul-Rahman