1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ziara ya George Mitchell nchini Israel

11 Septemba 2009

<p>Katika mabishano kuhusu kupatikana amani baina ya Israel na Wapalastina, Marekani inamtuma tena mwakilishi wake juu ya Mashariki ya Kati, George Mitchell, hadi eneo hilo.

https://p.dw.com/p/JdHa
Mwakilishi wa Marekani katika mashariki ya kati, George Mitchell (kushoto) pamoja na waziri mkuu wa Israel, Benjamin NetanyahuPicha: AP
Kutoka kesho, jumapili, hadi jumanne atafanya mazungumzo huko.Marekani inafanya juhudi za kutaka yarejewe tena mashauriano ya amani ya Mashariki ya Kati. Pia inaitaka Israel isitishe kujenga makaazi ya Wayahudi katika maeneo ya Wapalastina. Waziri wa ulinzi wa Israel, Ehud Barak, mwanzoni mwa wiki hii alitoa kibali cha kujengwa fleti 455 katika makaazi ya Wayahudi ambayo hivi sasa yako katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. 

Kabla hata hajawasili mwakilishi wa Marekani juu ya amani ya Mashariki ya Kati, George Mitchell, huko Israel, waziri mkuu wa nchi hiyo, Benjamin Netanjahu, aliwahakikishia walowezi wa Kiyahudi katika  ardhi zilizotekwa na Israel katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan kwamba hata baada  ya kurejewa tena mashauriano ya amani baina ya nchi yake na Wapalastina, Wayahudi hao wataweza kuishi maisha ya kawaida. Mbele ya wafuasi wa Chama chake cha Likud cha mrengo wa kulia, alisema:

"Nataka kuichukuwa nafasi hii kuwaambia ndugu zetu wapenzi wanaoishi katika Judea na Samaria, anakusudia maeneo ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Nyinyi ni raia wa kweli wa dola ya Israel na mna haki ya kuwa na maisha ya kawaida. Tutafanya mambo mawili wakati mmoja- tutasonga mbele na mwenendo wa kisiasa na kukuwezesheni nyinyi kuendesha maisha ya kawaida."

Mkuu huyo wa serekali ya Israel alisisitiza upya kwamba Jerusalem ya Mashariki iliotekwa na Israel katika vita vya siku sita baina ya Israel na nchi za Kiarabu hapo mwaka 1967 na baadae kutwaaliwa na Israel halitakuwa suala la mashauriano. Benjamini Netanjahu alisema mji wa Jerusalem ulioungana ni mji mkuu wa Wayahudi na utakuwa hivyo, tena maisha. Wapalastina wanadai sehemu ya Mashariki ya mji huo kama mji mkuu wa dola yao ya baadae.

Mwakilishi wa Marekani juu ya amani ya Mashariki, George Mitchell, anatarajiwa kuwasili leo jioni huko Israel ili kuandaa uwezekano wa kufanyika mkutano wa kilele baina ya Rais Barack Obama wa Israel, waziri mkuu Benjamain Netanyahu na Rais wa Wapalastina, Mahmud Abbas, mnamo wiki mbili zijazo huko New York. Hii ni kwa ajili ya nia ya kuyarejea tena mashauriano ya amani, alisistiza Netanyahu:

"Maisha tumetoa ushahidi kwamba tunataka amani, kwamba tuko tayari kuregeza kamba kuifikia amani. Lakini hatuko tayari kupelekwa njia nyingine, au kwa lugha ya kawaida, hatuko tayari kuuzwa na kufanywa wajinga. Kuna mambo ambayo hatuwezi kuachana nayo- kutambuliwa wazi na kinaga ubaga kwa haki ya Wayahudi kuwa na dola yao wenyewe katika ardhi ya Israel."

Kwa mujibu wa gazeti la kila siku la Israel, Ha'aretz, Mahmud Abbas ameiarifu Ikulu ya Marekani huko Washington pamoja na serekali za nchi za Ulaya kwamba yeye atashiriki tu katika mkutano huo pale Israel itakaposimamisha kabisa ujenzi ya makaazi ya Wayahudi katika Jerusalem ya Mashariki na katika ardhi zilizotekwa za Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Uamuzi wa Israel mwanzoni mwa wiki hii kutoa vibali vya kujengwa fleti mpya 450 za walowezi wa Kiyahudi ni moja ya mambo yaliomfanya Mahmud Abbas kutake kujitenga na mkutano huo wa pande tatu huko New York.

Rais wa Israel, Shimon Perez anajitahidi, kwa mujibu wa ripoti zaidi za gazeti la Ha'aretz, kumshawishi kiongozi wa upinzani, Tzipi Livni wa  Chama cha Kadima, ajiunge na serekali ya  umoja wa taifa ya mrengo wa kulia inayoongozwa na Benjamini Netanjahu. Shimon Perez amehakikisha kwamba Netanjahu yuko tayari kusitisha ujenzi wa makaazi katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na papo hapo kurejea upya kufanya mashauriano na Mahmud Abbas. Kwa mujibu wa maneno yake mwenyewe   Bibi Livni, yeye anakataa kujiunga na serekali ya mseto inayoongozwa na waziri mkuu Benjamin Netanjahu.

Mwandishi:Verenkotte Clemens/ZR/  Othman Miraji

Mhariri:M.Abdul-Rahman