1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ziara ya Jose Eduardo dos Santos Afrika Kusini

14 Desemba 2010

Rais wa Angola Jose Eduardo Dos Santos afanya ziara ya kwanza nchini Afrika Kusini.

https://p.dw.com/p/QYcO
Rais wa Angola, Jose Eduardo dos Santos .Picha: picture-alliance / dpa

Rais wa Angola Jose Eduardo dos Santos hii leo ameanza ziara rasmi ya kihistoria na ya  kwanza nchini Afrika kusini. Ziara hii imenuiwa kumaliza uhasama wa miongo kadhaa kati ya nchi hizo mbili zilizo kubwa katika eneo hilo kiuchumi.

Ziara ya rais Santos inafuata ile aliyoifanya mwenyeji wake rais Jacob Zuma wa Afrika kusini mwaka uliopita 2009 nchini  Angola yenye utajiri wa mafuta na mali nyengine za asili  na hali hiyo ililainisha msimamo wa Angola baada ya miongo kadhaa ya mvutano katika uhusiano wakati wa ubaguzi wa rangi na miaka ya awali ya utawala wa wingi wa watu weusi.

Viongozi hao wawili walikutana katika mji mkuu Pretoria  na wamefanya mazungumzo na kutia saini makubaliano ya nishati, mawasiliano  na ujenzi ikiwa  ni  katika siku ya kwanza ya ziara ya siku mbili inayonuiwa kuimarisha uchumi kati yao.

Süsafrika Jacob Zuma nach der Wahl
Rais wa Afrika kusini, Jacob Zuma.Picha: AP

Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma, amesema ziara hiyo ya Dos Santos imeimarisha ile enzi ya mapambano ya pamoja na hatimae kuundwa upya kwa  jamii mpya  katika nchi zote mbili .

Zuma amesema ziara hiyo itaingia katika kumbukumbu za vitabu vya kihistoria kama sehemu ya mwisho ya kuimarisha uhusiano kati ya nchi hizo mbili ambazo zitasalia kuunganishwa kwa historia ya vita, kujitolea kwao, na jitihada zao za pamoja za kupigania uhuru, haki na mustakbali mwema.

Alipongeza pia jukumu la Dos Santos  katika kukiunga mkono chama kilicho pigana dhidi ya  sera za  ubaguzi wa rangi nchini Afrika kusini, cha ANC kwa muda  mrefu kabla hakijaingia madarakani kufutia kumalizika kwa ubaguzi wa rangi  mwaka 1994.

Uhusiano kati ya nchi hizo mbili uliharibika  katika karne hiyo ya ubaguzi wa rangi, ambapo Afrika kusini iliwaunga mkono waasi wa UNITA waliokuwa wakipigana na chama cha Dos Santos  MPLA wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Lakini licha ya Dos Santos kuwaunga mkono baadhi ya viongozi wa ANC waliokwenda uhamishoni, hapakuwa na ushirikiano wa karibu wa mara moja wa kidiplomasia  wakati utawala wa wazungu  ulipokwisha  nchini Afrika kusini.

Waliokuwa marais wa nchi hiyo, Nelson Mandela na Thabo Mbeki, walipendekeza majadaliano na maafikiano katika vita vya kiraia vya Angola, lakini hatua hiyo Dos Santos aliipinga  hadi vita hivyo vilipokwisha mnamo mwaka 2002.

Chini ya Utawala wa Mbeki,  mataifa hayo mawili pia yalizozana kuhusu jinsi ya kuushughuliia mzozo wa Zimbabwe na ule wa  Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Pamoja na hayo Dos Santos leo aliyapongeza majukumu ya rais Nelson Mandela na  mtu aliyekua kivutio kikubwa kwake , rais wa zamani wa wa  ANC marehemu Oliver Tambo, na pia   rais wa zamani wa  Angola marehemu Agostinho Neto, katika kuleta mabadiliko katika nchi hizo mbili. Ziara ya  Rais dos Santos inamalizika kesho ambapo  atalitembeleza gereza  alikofungwa Mandela kwa miaka 18, katika kisiwa cha Robben  huko Cape Town.

Mwandishi:Maryam Abdalla/AFPE

Mhariri: Abdul-Rahman