1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ziara ya Kiongozi wa kidini wa Tibet Dalai Lama Ujerumani

Abdulrahman, Mohamed16 Mei 2008

Mivutano baina ya wanasiasa wa vyama vinavyounda katika serikali kuu mjini Berlin kuhusu ziara hiyo

https://p.dw.com/p/E16P
Dalai Lama akizungumza na Waziri mkuu wa Mkoa wa North Rhine Westphalia Juergen Ruettgers .Picha: picture-alliance/ dpa

Kiongozi wa kiroho wa Tibet aliwasili jana kwa ziara ya siku tano Dalai Lama nchini Ujerumani, akisisitiza kwamba utamaduni wa mchanganyiko wa Tibet pamoja na maadili yake ya utajiri mkubwa katika dini ya Buddha, ni mambo yanayosisitiza umuhimu wa kuwepo kwa utawala wa kweli wa ndani kuweza kujiamulia mambo yake yenyewe ya ndani ya China ilio moja.

Katika ziara hii Dalai Lama amepangiwa mikutano na wanasiasa kadhaa akipanga pia kutoa mihadhara minne kabla ya hotuba yake ya mwisho Jumatatu ijayo kwenye lango la Brandenburg mjini Berlin. Aidha mshindi huyo wa tunzo ya amani ya Nobeli 1989,amesha onana na Mawaziri wakuu wawili wa mikoa kutoka chama cha Christian Democrats CDU cha Kansela Angela Merkel ambao ni Juergen Ruettgers wa North Rhine-Westphalia na Rolandt Koch wa mkoa wa Hesse, pamoja na Spika wa bunge la Ujerumani Norbert Lammert.

Wakati akiwasili kiongozi huyo wa kidini wa Tibet alisisitiza kwamba anachopigania na malaka ya utawala wa kweli wa ndani wa Tibet na kusema hilo halinabudi kufikiwa bila matumizi ya nguvu. Akaongeza kwamba Tibet na China zina urithi wa pamoja wa utamaduni na mambo mengine, akiongeza kwamba anachopigania zaidi ni heshima ya binaadamu.

Lakini ziara yake hapa Ujerumani kwa upande mwengine imezusha mivutano miongoni mwa wanasiasa ndani ya serikali ya mseto baina ya CDU na Wasocial democrats SPD. Waziri mkuu wa mkoa wa Hesse Ronald Koch amemkosoa tena waziri wa mambo ya nchi za nje Frank-Walter Steinmeier kutoka chama cha SPD kwa uamuzi wa kutokutana na Dalai Lama wakati wa ziara hii. Akizungumza katika toleo la leo la gazeti la" Neuen Presse", Bw Koch alisema hatua hiyo inaashiria kutoeleweka kwa sera ya serikali ya Ujerumani kuhusiana na haki za binaadamu.

Wakati huo huo akapongeza mkutano unaopangwa kufanyika Jumatatu kati ya Dalai Lama na Waziri wa misaada ya maendeleo Bibi Heidemarie Wieczoek-Zeul akisema uamuzi wa mwanasaiasa huyo wa SPD ni wa kijasiri.

Dalai Lama hatokutana pia na Kansela Merkel ambaye kwa wakati huu yuko mjini Lima -Peru akihudhuria mkutano mkuu wa Viongozi wa Amerika kusini na nchi za Umoja wa Ulaya unaoanza leo.

Baadhi ya wanasiasa na wadadisi wameikosoa sera ya serikali ya Ujerumani kuelekea China, wakisema inaligubika suala la ukiukaji wa haki za binaadamu na kutoa kipa umbele kwa masilahi ya kiuchumi kwa sababu ya umuhimu wa China kibiashara. Ubalozi wa China mjini Berlin umetoa taarifa ukilalamika juu ya mkutano huo kati ya Bibi Wieczorek-Zeul na Dalai Lama.

Taarifa ya ubalozi huo imesema pamoja na kwamba China inataka kuzungumza na Ujerumani kuhusu Tibet lakini ni lazima sera ya China ilio moja izingatiwe na kuimarishwa. Mkutano kama huo mwaka jana baina ya Kiongozi huyo wa kidini wa Tibet na Kansela Merkel ulizusaha msuko suko kidogo katika uhusiano kati ya Berlin na Beijing.

Leo Dalai Lama amepangiwa kutoa mhadhara katika kituo cha mikutano mjini Bochum juu ya haki za binaadamu na utanda wazi.