1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ziara ya Malkia Elizabeth wa pili Ujerumani

24 Juni 2015

Malkia Elizabeth wa pili wa Uingereza na mumewe Philip, leo wanatimiza siku yao ya pili ya ziara ya siku tatu nchini Ujerumani. Atakaribishwa rasmi leo hii, na rais wa Ujerumani pamoja na kansela wa Ujerumani.

https://p.dw.com/p/1FmdG
Deutschland Queen in Berlin bei Gauck mit Publikum
Malkia Elizabeth wa pili wa Uingereza na rais wa Ujerumani Joachim GauckPicha: Reuters/M. Schreiber

Malkia Elizabeth wa Uingereza aliyewasili jana kwa ziara ya siku tatu akiwa na mumewePhilip, leo anatimiza siku yake ya pili baada ya jana kukaribishwa kwa heshima na jeshi la Ujerumani mjini Berlin. Leo hii wanatarajiwa kukutana na Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, ambae pia anajulikana kama Malkia wa Ulaya. Pia miongoni mwa ratiba ya ziara hiyo, atatembelea kambi ya mateso ya Wanazi iliyokombolewa na wanajeshi wa Kiingereza wakati wa kumalizika kwa vita vya pili vya Dunia mwaka 1945.

Malkia Elizabeth mwenye umri wa miaka 89, na mumewe Philip wa miaka 94, wanafanya ziara hiyo katika kipindi ambapo Uingereza inatafuta uungwaji mkono wa Ujerumani nchi yenye nguvu kubwa kiuchumi katika kanda ya euro, kuhusu mageuzi yanayodaiwa na Uingereza ndani ya Umoja wa Ulaya . Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron pia anatarajiwa kukutana na Kansela Merkel hii leo, kabla ya mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya utakaofanyika baadae wiki hii.

Deutschland Queen in Berlin bei Merkel
Malkia Elizabeth wa pili wa Uingereza na kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: Getty Images/AFP/R. Michael

Halikadhalika, rais wa Ujerumani Joachim Gauck atamkaribisha rasmi malkia Elizabeth na mumewe leo hii katika kasri lake la Bellevue.

Malkia kuzuru kambi ya Bergen-Belsen

Katika ziara yake hio malkia Elizabeth pia atahudhuria karamu ya kitaifa, na baadae atatembelea mji wa magharibi mwa Ujerumani wa Frankfurt. Pia atatembelea eneo la kihistoria mjini Berlin mahala lilipo lango maarufu na kihistoria la Brandenburg .

Kesho Malkia huyo na mumewe watatembelea iliyokuwa kambi ya mateso ya wanazi ya Bergen-Belsen, ambayo ilikombolewa kutoka kwa wanazi na jeshi la Uingereza mwaka 1945 mwisho wa vita vya pili vya dunia. Pia malkia Elizabeth atawatembelea manusura wa kambi hio ambapo kulifanyika mauwaji ya halaiki ya wayahudi ya Halocaust, pia atakutana na wanajeshi waliosaidia kuikomboa kambi hio ambapo wafungwa wa vita takriban 20,000 walifariki.

Mwanajeshi wa zamani aliyesaidia katika kuikomboa kempu ya Bergen-Belsen Bernard Levy mwenye umri wa miaka 89, amesema kuwa ni vyema kwa Malkia huyo kuzuru kambi hiyo. Aliongeza kuwa elimu juu ya mauwaji ya halaiki ya wayahudi ya Halocaust ni muhimu. Hasa kwa watoto wa miaka ya leo, wengi hawajui yaliyotokea. Ziara ya Malkia itaonesha umuhimu wa matukio yaliyotokea katika kambi hio.

Hii ni ziara ya tano kwa Malkia Elizabeth wa pili na mumewe Philip, walishawahi kuizuru Ujerumani mara nne.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/afpe/dw

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman