1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ziara ya Rais Bush kuaga Ulaya

P.Martin16 Juni 2008

Rais George W. Bush wa Marekani anaendelea na ziara yake ya kuiaga Ulaya kabla ya kuondoka madarakani Januari 2009.

https://p.dw.com/p/EKgN
Britain's Prime Minister Gordon Brown, left, poses with US President George W. Bush, on the doorstep of his official residence at !0 Downing Street in central London, prior to their meeting, Monday June 16, 2008. US President Bush and his wife Laura are on a two-day trip to England. (AP Photo/Lefteris Pitar
Rais wa Marekani George W.Bush(kulia) pamoja na Waziri Mkuu wa Uingereza Gordon Brown kabla ya kuhudhuria mkutano na waandishi wa habari Juni 16,2008 mjini London.Picha: AP

Bush amefurahishwa na ahadi zilizotolewa na serikali ya Uingereza kuimarisha vikwazo dhidi ya Iran na kupeleka vikosi zaidi Afghanistan ambako machafuko yanazidi kushika kasi.

Bush na Waziri Mkuu wa Uingereza Gordon Brown waliutumia mkutano wao,pamoja na waandishi wa habari kuonyesha mshikamano katika sera za nje kwenye masuala ya utata:hasa Iran,Iraq,Afghanistan na bila shaka Zimbabwe pia.

Upande wa Iraq,Bush amesema,yeye hana matatizo na msimamo wa Brown katika suala la kupunguza vikosi huko Iraq.Ameusifu msimamo wa Brown kupiga vita ugaidi pamoja na uzatiti wake kupambana na wanamgambo wa Taliban nchini Afghanistan.

Katika suala linalohusika na mradi wa nyuklia wa Iran viongozi hao wawili wametoa wito kwa Tehran kutochagua njia ya mapambano.Hata hivyo wamesema,Iran itawekewa vikwazo vikali zaidi ikiwa itaendelea kungangania msimamo wake mkamavu kuhusu mradi wake wa nyuklia.

Bush na Gordon walikuwa na msimamo mmoja pia kuhusu Zimbabwe.Wametoa wito kwa Rais Robert Mugabe kuwaruhusu waangalizi wa kimataifa ili kuhakikisha kuwa uchaguzi utakaofanywa Juni 27 utakuwa huru na wa haki.Bush amesema Marekani ipo tayari kutoa msaada wake kuhakikisha uchaguzi wa haki nchini Zimbabwe.

Lakini ziara ya Bush barani Ulaya hasa ilitoa umuhimu zaidi kwa masuala ya Mashariki ya Kati na hii leo alikutana na rafiki yake aliekuwa waziri mkuu wa Uingereza,Tony Blair ambae hivi sasa ni mjumbe wa kimataifa katika masuala ya Mashariki ya Kati.

Yadhihirika kuwa Bush ameridhika na uungaji mkono aliyopata katika ziara yake ya kuaga Ulaya,kinyume na waziri wake wa nje Condoleezza Rice aliekuwa Mashariki ya Kati kwa ziara ya siku mbili.Kwani Rice ameikamilisha ziara hiyo katika Mashariki ya Kati bila ya kuona ishara ya kupatikana makubaliano ya amani kati ya Waisraeli na Wapalestina ifikapo mwisho wa 2008.Kilichomvunja moyo zaidi ni tangazo la serikali ya Israel kuwa itajenga nyumba mpya 1,300 huko mashariki mwa Jerusalem.Condoleezza Rice alilikosoa vikali tangazo hilo kwa kusema:

"Mimi na Marekani tunaamini kuwa vitendo na matangazo ya hivi karibuni yanachafua mazingira ya majadiliano - na hicho sicho tunachokitaka.Tunapaswa kuhimiza imani na siyo kupunguza."

Lakini Waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert amepuza lawama hizo na amesema,Israel itaendelea na ujenzi huo. Kwa upande mwingine,Wapalestina wanasema,mji wao mkuu utakuwa Jerusalem ya Mashariki patakapoundwa taifa la Palestina.

Ni dhahiri kuwa ujenzi wa nyumba zaidi za walowezi katika Ukingo wa Magharibi pamoja na kashfa ya rushwa inayomkabili Olmert na kuhatarisha kiongozi huyo kuondoshwa madarakani,ni pigo kwa juhudi za Rais Bush kupata makubaliano ya kuunda taifa la Palestina kabla ya kuondoka madarakani Januari 2009.