1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ziara ya rais Mursi wa Misri nchini Ujerumani

31 Januari 2013

Mada kuu magazetini ni ziara ya Rais Mohammad Mursi wa Misri nchini Ujerumani. Hata hivyo hata madai ya kusengenywa mwandishi habari wa kike na mkuu wa kundi la wabunge wa chama cha FDP Rainer Brüderle yamezingatiwa

https://p.dw.com/p/17V4W
Kansela Merkel na rais Mursi wakikutana mjini BerlinPicha: dapd

Tuanzie lakini Berlin na ziara ya Rais wa Misri, Mohammed Mursi. Gazeti la Rheinpfalz linaandika:Ujerumani inalazimika kuikosowa Misri. Mfuasi huyo wa zamani wa udugu wa kiislam anabidi kuhakikisha kwamba yeye ni mshirika wa kuaminika ulimwenguni. Kwamba uwezo huo anao, amebainisha katika mzozo wa hivi karibuni wa Gaza. Lakini msimamo wake jumla kuelekea Israel haukubaliki na wala si wa busara. Rais wa Israel Perez alimwalika Mursi mara baada ya kukabidhiwa hatamu za uongozi nchini mwake, aitembelee Israel. Hadi wakati huu, kwa mujibu wa serikali ya Israel, sio tu hakuna jibu lolote kutoka Cairo, bali pia Mursi anakwepa hata kulitaja neno Israel. Hali hiyo inafanya iwe shida watu kuamini kikamilifu aliposema ataheshimu makubaliano yote yaliyofikiwa.


Kansela Angela Merkel ameepuka lawama kali kali na badala yake alimtolea mwito Rais Mursi azidi kupigania demokrasia kwa njia ya amani. Mursi ameahidi kuharakisha mageuzi ya kidemokrasia. Lakini ahadi amezitoa nyingi tu mfuasi huyo wa Udugu wa Kiislamu. Alichotekeleza ni ahadi moja tu nayo ni ile ya kuharakisha kuunda taifa la Kiislamu.

FDP Matatani

Rainer Brüderle und Laura Himmelreich
Rainer Brüderle na mwandishi habari Laura Himmelreich kabla ya madai ya kusengenywa kuchapishwaPicha: picture-alliance/dpa

Mada nyengine magazetini inahusiana na mjadala uliozushwa na madai kwamba eti mwenyekiti wa wabunge wa chama cha kiliberali hapa Ujerumani, FDP, Rainer Brüderle amemsengenya mwandishi habari mmoja wa kike wa jarida la "Stern". Jana katika mkutano pamoja na waandishi habari mjini Berlin, waandishi walifikiria kisa hicho kingefafanuliwa. Kilichotokea ni chengine kabisa. Rainer Brüderle ameamua kutosema chochote. Gazeti la "Rhein-Zeitung" linaandika:

Kunyamaza kimya kiongozi mpya wa waliberali Rainer Brüderle,miezi michache kabla ya uchaguzi mkuu, kutakisababishia matatizo chama hicho. Jina lake linafungamanishwa hivi sasa na madai ya kusengenywa watu kwaajili ya jinsia yao. Hilo haliwezi kuwa jambo la maana sio kwake yeye na wala si kwa chama chake. Brüderle anawaacha wapiga kura wasiovutiwa hata kidogo na mchanganyiko wa mbinu za kisiasa na vyombo vya habari katika hali ya kutojua nini hasa kimetokea.

Nalo gazeti la Mannheimer Morgen linamalizia:Mjadala uliozushwa na madai ya kusengenywa mwandishi habari wa kike kwa sababu ya jinsia yake umegubika matokeo ya kustaajabisha katika uchaguzi wa Lower Saxony. Tangu kisa hiki kilipojulikana tafiti zote za maoni ya umma zinaonyesha chama cha FDP kinapotelewa na wapiga kura.Ingawa imesalia miezi minane hadi uchaguzi mkuu, lakini suala watu wanalojiuliza mpaka sasa halijapatiwa jibu. Brüderle atakaeshika bendera ya chama hicho katika auchaguzi mkuu anaonyesha kudhoofika licha ya matokeo ya Lower Saxony.

Mwandishi: Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Mohammed Khelef