1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ziara ya Rais wa Israel Peres, Berlin

27 Januari 2010

Mkutano wake na Kanzela Merkel

https://p.dw.com/p/LhkX
Peres na Merkel (Berlin)

MERKEL AKUTANA NA PERES BERLIN

Kanzela Angela Merkel wa Ujerumani, alikutana jioni na Rais Shimon Peres wa Israel alie katika ziara ya siku 3 nchini Ujerumani.Katika ajenda ya mazungumzo yao miongoni mwa yale waliozungumza, ni mradi wa nuklia wa Iran na hali katika Mashariki ya Kati.Leo, rais Peres anahutubia kama rais wa kwanza wa Israel Bunge la Ujerumani-Bundestag.

MRADI WA IRAN WA KINUKLIA

Iran na mradi wake wa nuklia ilikuwa katika kitovu cha ajenda ya mazungumzo hapo jana kati ya Kanzela Angela Merkel na Rais Shimon Peres wa Israel.Merkel alisema wakati kwa Iran unapita.Jamii ya kimataifa imeonesha subira kubwa na imeinyoshea mkono Iran tena na tena kufikia nayo suluhu.Sasa wakati umewadia kuiwekea vikwazo vya kiuchumi-alisema kanzela Merkel:

"Natazamia kuwa chini ya wenyekiti wa Ufaransa wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwezi ujao wa februari,mada hii itawekwa mezani.Tunaiungamkono Ufaransa ikiwa mwenyekiti wa Baraza la Usalama na ndio maana, naamini, kuwa mwezi ujao wa Februari, utakuwa wa kusisimua kuelekea shabaha hiyo."

Kutokana na swali alilouliza mwandishi habari wa kiisrael,iwapo bibi Merkel yutayari pia kuungamkono hata hatua za kijeshi dhidi ya Iran ,Bibi Merkel alijibu kwamba, Ujerumani itaendelea kuungamkono juhudi za kidiplomasia.Lakini haikubaliki kabisa, aliongeza, msimamo inaochukua Iran mbele ya Israel. Bibi Merkel akasema na ninamnukulu,

"Kuwa kila mara rais wa Iran anakanusha kuwa Israel haina haki ya kudumu kama dola, ni jambo lisilokubalika kwa kanzela wa Ujerumani na tena na tena nikiweka wazi ni sehemu ya sera za dola letu kutetea usalama na mustakbala wa Israel."

Nae Rais Perez alisema,

"Hatupigani na Iran,bali na udikteta nchini Iran.Kwani, serikali ya sasa ya Iran ni hatari na ya udikteta.Inawaua watu wasio na hatia na inaweka pingamizi kwa amani katika Mashariki ya Kati."

MASHARIKI YA KATI:

Kuhusu mzozo wa Mashariki ya Kati,rais Peres, alisema nchi yake itayari kuwasaidia wapalestina ili kujiendeleza kiuchumi kama daima ikifanya.Kwa waisraeli na wapalestina,alisema , hakuna njia nyengine isipokuwa ufumbuzi wa dola mbil.Kanzela Merkel hakukosoa sera za serikali ya Israel,isipokuwa alimpongeza mgeni wake rais Peres kuwa daima akiungamkono ufumbuzi wa amani wa mgogoro wa Mashariki ya Kati.Nae rais Peres akarejesha pongezi nyingi kwa mwenyeji wake bibi Merkel:

"Nimekuja na salamu za heshima kubwa kwako bibi Kanzela.Tunakuona ni rafiki mkubwa wa nchi yetu na tunauamini msimamo wako, tumevutiwa na kutoyumbayumba kwako; na tunathamini mno msimamo wako ulio wazi na usio-regarega."

Rais Peres hii leo, analihutubia Bunge la Ujerumani-Bundestag, akiwa rais wa kwanza wa Israel kufanya hivyo.

Mwandishi: Marx,Bettina (DW Berlin)

Mtayarishi:Ramadhan Ali

Uhariri: Othman Miraji