1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Steinmeier afanya mazungumzo Washington

Abdu Said Mtullya3 Februari 2009

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier yupo nchini Marekani kwa ajili ya mazungumzo na waziri mwenzake Hillary Clinton.

https://p.dw.com/p/Gmca
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier.Picha: AP


Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank Walter- Steinmeier yupo Marekani kwa ajili ya mazungumzo na waziri mwenzake Hillary Clinton.Mawaziri hao wanatarajiwa kuzungumzia masuala ya usalama,uchumi na uhusiano baina ya nchi zao.Mawaziri hao pia watajadili suala la upunguzaji wa silaha na uhusiano baina ya Urusi na Marekani.

Waziri Steinmeier amesema masuala kama hayo ni rahisi kuyajadili na utawala mpya wa Marekani. Waziri Steinmeier pia atajadili na waziri mwenzake wa Marekani Hillary Clinton juu ya Iran na Afghanistan.

Mazungumzo ya mawaziri hao yanafanyika kabla ya mkutano wa kesho mjini Berlin wa wawakilishi wa Ujerumani na wa nchi wanachama wa kudumu kwenye baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.Wawakilishi hao watajadili mzozo wa nyuklia na Iran kwenye mkutano wao.

Kwenye mazungumzo yao mjini Washington leo ,mawaziri Steinmeier na mwenzake Hillary Clinton pia watajadili mgogoro wa uchumi, nishati, mabadiliko ya hali ya hewa na hali ya nchini Irak.Mazungumzo yao pia yatahusu mgogoro wa mashariki ya kati, husasan baada ya vita vya Gaza.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Ujerumani ameeleza kuwa ziara ya waziri Steinmeier pia inalenga shabaha ya kujadili masuala ya ndani ya Ujerumani.

Ujerumani pia imekuwa inafuatilia kwa makini dhamira ya Marekani ya kuifunga jela yake ya kijeshi ya Guantanamo.Mjadala unaendelea nchini Ujerumani iwapo, baadhi ya wafungwa watakaoachiwa watapewa hifadhi nchini Ujerumani.

Marekani ambayo inakusudia kuifunga jela hiyo hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu haijatoa maombi rasmi kwa Ujerumani juu ya kuwachukua wafungwa hao.