1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Diplomasia ya kimya kimya

9 Machi 2015

Ziara ya waziri wa uchumi wa serikali kuu ya Ujerumani,S Gabriel nchini Saud Arabia,na pendekezo la mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya la kuwa na jeshi la nchi za Umoja huo ni miongoni mwa mada magazetini

https://p.dw.com/p/1EnWK
Waziri wa uchumi wa Ujerumani Sigmar Gabriel akiamkiana na mfalme Salman bin Abdelaziz wa Saud ArabiaPicha: picture-alliance/dpa/Bernd von Jutrczenka

Tuanzie lakini katika Ghuba la Uajemi ambako waziri wa uchumi,makamo kansela wa Ujerumani Sigmar Gabriel alikuwa ziarani nchini Saud Arabia.Nasaha yake ya kutaka aachiliwe huru mwanablogi Raif Baddawi imekataliwa na watawala wa nchi hiyo ya kifalme.Gazeti la "Mannheimer Morgen" linahimiza jibu linalostahiki na kuandika:"Jinsi viongozi wa Saud Arabia walivyolikataa pendekezo la Gabriel la kutaka aachiliwe huru Badawi,inamaanisha mengi,na kwa namna hiyo jibu pia linabidi lifuate.Ikiwa makampuni ya silaha ya Ujerumani yatataka kuendelea kuwauzia zana zao watawala wa kibamavu wa Riyadh- jambo ambalo tokea hapo linaudhi,kipi kitazuwia ikiwa biashara hiyo itafungamanishwa siku za mbele na hali bora ya kuheshimiwa haki za binaadam?Fedha au mfereji wa mafuta kuelekea Ujerumani,wasaudi hawataufunga kwasababu hiyo.Wanataka pia kufanya biashara sawa na wajasiria mali waliofuatana na Gabriel mjini Riyadh.Ili kuwepo na ushirika sawia-kama anavyosema waziri wa uchumi,wakujirekebisha si shirikisho la jamhuri ya Ujerumani,bali Saud Arabia.

Diplomasia ya kimya kimya ni bora zaidi

Gazeti la Stuttgarter Zeitung linahisi wakukosolewa ni mwenyewe waziri wa uchumi.Gazeti linaendelea kuandika:"Kwamba mfalme wa Saud Arabia amepitisha dakika 90 kuzungumza na waziri wa uchumi Sigmar Gabriel,ni ushahidi wa jinsi Ujerumani inavyothaminiwa katika eneo hilo.Kutokana na hayo,haikuwa busara kwa Gabriel kufichua katika mahojiano hata kabla ya ziara yake,kile anachopanga kumwambia mfalme kuhusiana na kadhia ya Badawi.Ikiwa serikali kuu ya Ujerumani inataka kweli kusaidia,itabidi izingatie kwamba mshirika wake mazungumzoni anaweza kuhifadhi hadhi yake.Maarifa yameonyesha juhudi za kimya kimya ndizo zinazoleta tija zaidi.

Wazo la kuundwa jeshi la ulaya si jipya

Mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa ulaya Jean-Claude Juncker amependekeza liundwe jeshi la nchi za Umoja huo.Fikra hiyo si mpya linaandika gazeti la "Flensburger Tageblatt:"Changamoto katika sera za usalama zinazidi kuwa za jumla.Nchi moja moja hazina tena uwezo wa kuyapatia ufumbuzi matatizo yanayozidi kukuwa.Ulaya yenye nguvu kijeshi,inaweza kusaidia.Lakini njia bado ni ndefu.Ni ndefu kwa namna ambayo watu wanaweza kufikiria utekelezaji wake hauwezekani.Hasa kwakua kwanza linabidi lipatiwe ufafanuzi suala la muundo wa uongozi kati ya jumuia ya kujihami ya NATO na jeshi la nchi za Umoja wa Ulaya.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman