1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zilzala nchini Chile na kadhia ya CDU kupokea fedha za wafadhili kichini chini

Oumilkher Hamidou1 Machi 2010

Wahariri walinganisha hali nchini Chile na ile ya Haiti iliyoathirika vibaya sana kwa tetemeko la ardhi lililopiga january mwaka huu

https://p.dw.com/p/MErE
Rais Michelle Bachelet wa Chile akitangaza hali ya hatari katika maeneo kadhaa ya nchi hiyo yaliyoathirika vibaya sana na tetemeko la ardhiPicha: AP

Tetemeko la ardhi nchini Chile, wafadhili wa vyama vya kisiasa na homa ya uchaguzi katika jimbo la North Rhine Westfalia ni miongoni mwa mada zilizotangulizwa mbele na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo.

Tuanzie lakini na tetemeko la ardhi nchini Chile ambapo gazeti la "Badische Zeitung" linaandika:

"Salama kwamba balaa la kwanza halijafuatiwa na la pili: Tsunami haikufikia kiwango kilichokua kikihofiwa na wakaazi wa maeneo yanayopakana na Bahari ya Pacific walikua wameshajiandaa. Cha kusisimua ni ule ukweli kwamba katika hali kama hii ya maafa, walimwengu wanaonyesha mshikamano, hata kama ni kwa muda mfupi. Jambo ambalo, kawaida na kwa bahati mbaya, ni nadra kushuhudiwa."

Gazeti la DRESDNER NEUESTE NACHRICHTEN linafungamanisha zilzala iliyopiga Chile na ile ya Haiti.Gazeti linaendelea kuandika:

"Janga lililotokea Chile linakumbusha lile lililotokea Januari mwaka huu nchini Haiti. Nchi zote mbili zinakutikana katika eneo la kitisho kikubwa zaidi cha matetemeko ya ardhi. Lakini badala ya watu zaidi ya laki mbili na 20 elfu waliofariki dunia nchini Haiti, nchini Chile, kwa bahati nzuri, waliopoteza maisha yao ni watu mia kadhaa tuu.Majumba mengi yamejengwa kwa kuzingatia kinga dhidi ya tetemeko la ardhi. Kuna mipango ya dharura na idara maalum inayosimamia maafa pindi yakitokea. Si makosa ya wananchi wa Haiti kama hali haikua hivyo nchini mwao. Ndio maana watahitaji msaada kutoka nje kwa muda mrefu hadi watakapofarajika kidogo."

Mada yetu ya pili inahusu kisa cha kupokea fedha chama cha CDU katika jmaimbo ya North Rhine Wesfalia na Sachsen.Gazeti la "Bild Zeitung la mjini Berlin linaandika:

Jürgen Rüttgers
Waziri mkuu wa jimbo la North Rhine Westfalia Jürgen RüttgersPicha: AP

Katika jimbo la North Rhine Westfalia, sawa na katika jimbo la Sachsen, chama tawala cha CDU kinawavutia wafadhili wenye kutoa fedha nyingi kwa ahadi za kupata nafasi ya kuzungumza na mawaziri wakuu. Hapo hapo kuna wanaodhania kwamba wanasiasa wote wanaweza kununuliwa. Upuuzi mtupu. Bila ya shaka, hata katika siasa kuna wenye dosari, lakini nani anaeamini kwa dhati kwamba waziri mkuu au waziri tuu angepitisha uamuzi wake eti kwa sababu ya kumridhisha mfadhili tuu? Si hayo tuu,Jürgen Rüttgers au Stanislaw Tilich hawatawali kimabavu. Bila ya bunge,hawawezi kupitisha uamuzi wowote. Hata hivyo, hapa hakuna wa kumuonea huruma. Kwa sababu wao wenyewe ndio waliowaleta kazini wafuasi hao wa chama ambao kwa mkumbo mmoja wamewaharibia sifa zao viongozi wa chama chao na wanasiasa kwa jumla. Kinachoweza kusaidia hapo ni kimoja, nacho ni kupiga marufuku mitindo ya kugharimia vyama vya kisiasa kichini chini.

Mada yetu ya mwisho magazetini inaturejesha katika jimbo la North Rhine Westfalia ambako homa ya uchaguzi imeshaanza kupanda. Gazeti la "WESTDEUTSCHE ZEITUNG la mjini Düsseldorf linaandika:

Awamu moto moto ya kampeni ya uchaguzi itaanza baada ya siku kuu ya pasaka. Hapo macho ya wananchi wote wa shirikisho la jamhuri ya Ujerumani yatakodolewa katika jimbo la North Rhine Westfalia. Yule ambae hakumbwi na shinikizo lolote na hakufanya makosa makubwa ndie atakaeibuka na ushindi.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir

Imepitiwa na Othman, Miraji