1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zilzala ya kisiasa kwa chama cha CSU

Hamidou, Oumilkher29 Septemba 2008

Vyama vidogo vidogo vyaibuka na ushindi katika jimbo la kusini la Bavaria

https://p.dw.com/p/FQvA
Mpiga kura wa kike akivalia nguo za kiasili za BavariaPicha: picture-alliance/ dpa



Matokeo ya uchaguzi katika jimbo la Bavaria na nchini Austria ndiyo mada zilizotangulizwa mbele na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo.Lakini hata mpango wa serikali ya Marekani wa kunusuru uchumi haujaachwa kando.


Tuanzie lakini kusini mwa Ujerumani ambako gazeti la Die Welt linamulika matokeo mabaya kabisa kuwahi kukisibu chama cha Christian Social Union-CSU.Gazeti linaendelea kuandika:


"Hakuna tena chama cha taifa katika shirikisho la jamhuri ya Ujerumani.Kwanza walikua wana Social Democratic SPD waliopoteza madaraka yao yaliyodumu miongo kadhaa katika jimbo la North Rhine Westphalia na jana CSU nao wakapoteza enzi ya aina pekee waliyokua nayo katika jimbo la Bavaria.Kiroja cha matokeo hayo lakini ni kwamvba; ingawa  CSU kimejikingia kura ambazo kwengineko nchini Ujerumani chama chochote kile chengine kingeyashangiria kama ni ushindi mkubwa,kwao wao lakini wana CSU katika jimbo la Bavaria,matokeo hayo hayo ni ya aibu kubwa.Sifa ya chama cha Alfons Goppel,Franz Josef Strauß na Edmund Stoiber imechujuka.Vyama ndugu vya CDU/CSU vimepoteza madaraka ambayo ndiyo sababu iliyomfanya kansela Angela Merkel avipe kisogo viti vya upande wa upinzani uchaguzi mkuu ulipoitishwa mnmo mwaka 2005."


Die SCHWERINER VOLKSZEITUNG linahisi nguvu za wananchi zimesalia kama zamani.Gazeti linaendelea kuandika:


"Sauti zao zimetawanyika,hazituwami tena katika chama cha CSU kama ilivyokua zamani.Ndio maana FDP wameweza kushangiria bila ya jitihada yoyote ya maana.Hivi sasa kila kitu kina ashiria uwezekano wa kuundwa serikali ya muungano kati ya CSU na FDP katika jimbo la Bavaria.Ikiwa wafuasi wa nyeusi na njano wataungana,basi mtetezi wa kiti cha rais wa shirikisho Gesine Schwan atakua na shida,kwasababu wingi wa viti katika baraza la wawakiilishi wa majimbo hautabadilika.Wakati huo huo kansela Angela Merkel amepoteza nguzo  muhimu,kwasababu uchaguzi unapoitishwa wapiga kura wa Bavaria daima walikua wakielemea upande wa CDU/CSU.Kwa hivyo jana haikua siku ya msiba pekee kwa jimbo la Bavaria,bali kwa vyama ndugu vya CDU/CSU kiwa jumla."


Gazeti la MÜNCHNER MERKUR linahisi kwa upande wake:


"Msiba huu umesababishwa na mambo chungu nzima,lakini watu wawili wamechangia:Huber na Beckstein.Uongozi mpya umezidiwa na badala ya kukiinua chama cha CSU cha Stoiber wamekididimiza.Ndio maana wapiga kura wamewapa kisogo.Chama hicho kinakabiliwa hivi sasa na mtihani mkubwa.Wakiendelea na sera zao  watajikuta pia wakipotoleza kura  katika uchaguzi wa ulaya na pia uchaguzi mkuu hapo mwakani.Au wabadilishe uongozi na uvumi umezagaa kuhusu mapambano makali ya kuania madaraka ndani ya chama cha CSU."


Mada ya pili magazetini inahusu uchaguzi wa bunge nchini Austria.Gazeti la FRANKFURTER RUNDSCHAU linaandika:


"Haijawahi kutokea barani Ulaya tangu mwaka 1945,kuona chama cha siasa kali za mrengo wa kulia kinajikingia kura nyingi kupita kiasi,kama ilivyoshuhudiwa katika uchaguzi wa jana nchini Austria.Asili mia 29,kama mtu atahesabu kura za makundi yote mawili hasimu ya siasa kali za mrengo wa kulia.Ni kitandawili kikubwa hiki:sababu ya hali hiyo sio udhaifu wa demokrasia bali nguvu za siasa kali za mrengo wa kulia.Wapiga kura wao  wanataka "Utajiri wa Austria ugawanywe sawa na mgeni hastahiki kuuonja."Wanaotea ya miaka ya 70,sio ya miaka ya 30:pawepo taifa linalodhamini mahitaji ya jamii,hata kama wageni watakuwepo,muhimu lakini wanarejea makwao baada ya  wiki tatu."